Msando awataka waandishi kutete haki za binadamu
NA MADINA ISSA MKUU wa wilaya ya Morogoro, Albert Msando, amewataka wanahabari nchini kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi zikiwemo za utetezi wa haki za binadamu ili kuongeza tija katika kutoa habari kwa wananchi. Aliyasema hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wanahabari yanayohusu namna bora ya kutoa habari yaliyoratibiwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), yanayofanyika mkoani Morogoro. “Mwandishi wa habari mzuri ni yule anayetoa taarifa zinazozingatia ukweli, usahihi na kutopendelea ili jamii inufaike na wenye mamlaka wachukue hatua zinazostahiki,” alieleza Msando. Aidha aliwataka wanahabari kujitahidi kuwa watetezi wa haki za binadamu bila ya ushabiki au kuegemea upande mmoja ili kuepukana na changamoto mbali mbali zinazoweza kuwatokea. “Tujitahidini sana kuishi katika utetetezi wa haki za binaadamu na tusimameni katika ukweli na haki na wala tusiwe chanzo cha machafuko badala yake tuache habari ifike kama ilivyo ili wananchi ...