Msando awataka waandishi kutete haki za binadamu

NA MADINA ISSA

MKUU wa wilaya ya Morogoro, Albert Msando, amewataka wanahabari nchini kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi zikiwemo za utetezi wa haki za binadamu ili kuongeza tija katika kutoa habari kwa wananchi.

Aliyasema hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wanahabari yanayohusu namna bora ya kutoa habari yaliyoratibiwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), yanayofanyika mkoani Morogoro.

“Mwandishi wa habari mzuri ni yule anayetoa taarifa zinazozingatia ukweli, usahihi na kutopendelea ili jamii inufaike na wenye mamlaka wachukue hatua zinazostahiki,” alieleza Msando.

Aidha aliwataka wanahabari kujitahidi kuwa watetezi wa haki za binadamu bila ya ushabiki au kuegemea upande mmoja ili kuepukana na changamoto mbali mbali zinazoweza kuwatokea.

“Tujitahidini sana kuishi katika utetetezi wa haki za binaadamu na tusimameni katika ukweli na haki na wala tusiwe chanzo cha machafuko badala yake tuache habari ifike kama ilivyo ili wananchi wamue,” alieleza.

Alisema kuwa serikali ya awamu ya sita haina nia ya kuwanyima wanahabari uhuru wao wa kutoa habari na hakuna sababu ya kuishi kwa woga na kuwahimiza kuendelea kufanya kazi kwa mujibu wa misingi ya sheria na miongozo ya kihabari iliyopo.



Nae Jaji Mstaafu Robert Makaramba, alikiwasilisha mada ya namna ya kuandika na kuripoti habari za mahakamani, alisema kuwa ni vyema wakaepuka kutoa taarifa ambazo hazijatolewa mahakamani ili kuepusha sintofahamu kwenye jamii.

Jaji Makambara aliwataka waandishi wa habari kuzingatia taratibu na kanuni zilizopo huku akikiri kuwepo kwa baadhi ya sheria kandamizi ambazo, alishauri haja ya kufanyiwa marekebisho.

Awali akizungumza Wakili kutoka THRDC, Leopold Mosha, alisema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari juu ya namna ya kuandika na kuripoti taarifa zinazohusiana na haki za binadamu kutoka mikoa mbali mbali nchini.

Alisema THDRC imebaini kuwepo kwa changamoto mbali mbali katika kuripoti masuala yanayoendana na kisheria jinsi ya kutoa taarifa za kesi mahakamani na maamuzi ya kimahakama.

“Tulibaini kwamba taarifa nyingi zilikuwa zinatolewa na mapungufu ikiwemo kiufundi na zimekuwa zinaleta mkakasi katika jamii,” alieleza Wakili Mosha.

Hivyo, alisema kupatiwa mafunzo hayo, yatawawezesha wanahabari kujua vigezo na maeneo ya kisheria wanayopaswa kuzifuata wakati wanaporipoti kesi mbalimbali ambapo nchi ipo na sheria.

Kwa upande wake Afisa Uchechemuzi wa THRDC, Nuru Maro, akiwasilisha mada ya umuhimu wa waandishi wa habari katika kufanya uchechemuzi wa masuala mbali mbali alisema ni vyema waandishi kufahamu chanzo, ushahidi, kujua watu wengine wanavyofanya kazi hilo eneo husika.

Aidha alisema kuwa waandishi wa habari ni daraja la kuwaunganisha wannachi wote hivyo watumie kalamu zao ili kuona hali inaendelea kuwa nzuri na kufikisha ujumbe kwa jamii ukiwa na hali halisi na ukweli ndani yake.

Baadhi ya wanahabari wanaoshiriki mafunzo hayo, waliahidi kufanya kazi kwa mujibu wa sheria zilizopo sambamba na kuibua kitu mambo yatakayoleta mabadiliko katika utendaji na jamii kwa ujumla.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango