Hakuna habari yenye thamani zaidi ya maisha - Mussa

NA MWANDISHI WETU

WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kuzingatia usalama wao wanapokua katika kazi za kutafuta na kutoa habari.

Akifungua mafunzo ya ulinzi na usalama kwa waandishi wa habari, Mjumbe wa Bodi ya wakurugenzi ya muungano wa klabu za waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Yussuf Mussa, alisema mafunzo hayo yatawajengea uwezo waandishi kujitambua na kujua thamani yao katika utendaji wa kazi zao.

Alisema waandishi wa habari wana jukumu la kuwapasha wananchi habari lakini sayansi na teknolojia inawaweka wanahabari katika hatari licha ya kurahisisha kazi zao, hivyo ipo haja ya kujua jinsi ya kujilinda.

Awali Ofisa Programu, Machapisho, Utafiti na Mafunzo kutoka UTPC, Victor Maleko, alieleza kuwa suala la usalama na ulinzi wa waandishi ni muhimu hivyo ni vyema wakazingatia wanachofundishwa.


Aidha alisema UTPC inatekeleza mradi wa miaka miwili unaolenga kuzijengea uwezo taasisi za kihabari nchini, ambapo moja ya shughuli zake ni kutoa mafunzo kwa wanachama wa klabu kuhusu ulinzi na usalama kwa waandishi wa habari.

Mkufunzi wa mafunzo hayo, Mtaalamu wa Mawasiliano ya umma, Dk. Joyce Bazira, alisema sio vyombo vyote vinavyomsaidia mwandishi wa habari anapofikwa na matatizo na kuwataka kuwa makini wakati wanapotekeleza majukumu yao. 

Akiwasilisha mada ya namna ya kujilinda katika mitandao, Mkurugenzi Mkuu wa Tanzania Media Foundation (TMF), Dastan Kamanzi, aliwataka waandishi kuacha tabia ya kuweka taarifa zao binafsi kwenye mitandao, kwani zinaweza kuwarahisishia wahalifu wenye lengo la kuwadhuru.

Kwa upande wao waandishi walieleza kuwa, wamekuwa wakitishiwa usalama wa maisha yao hasa pale wanapoandika habari ambazo zinawagusa watu ambao hawatakii mema maslahi ya jamii yao, jambo ambalo linarudisha nyuma tasnia ya habari nchini.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na UTPC kwa kushirikiana na Shirika la International Media Support (IMS) la Denmark kupitia mradi wa usalama kwa waandishi wa habari unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU).

 

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango