ZAMECO yakumbushia sheria mpya ya habari

NA MWANDISHI MAALUM

KAMATI ya Wataalamu ya Vyombo vya Habari Zanzibar (ZAMECO), imeishauri serikali kukamilisha mchakato wa upatikanaji wa sheria mpya ya habari ili kuimarisha uhuru wa kujieleza na uwajibikaji.

Akizungumza wakati wa kongamano la maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani upande wa Zanzibar, lililofanyika Rahaleo Studio, Mjumbe wa ZAMECO, Salim Said Salim, alisema mchakato huo umechukua muda mrefu hivyo ipo haja ya kuchukuliwa kwa hatua za makusudi kuukamilisha.

“Katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia sheria nyingi zikipitishwa na Baraza la Wawakilishi ila sheria ya habari mchakato wake umekuwa ukienda na kurudi kwa zaidi ya miaka 20 hali inayowafanya wadau wa tasnia ya habari kujiona wanyonge”, alisema Salim.

BAADHI ya waandishi wa habari na wafdau wa habari wakifuatilia uwaasilishaji wa mada wakati wa kongamano 

Aliziomba mamlaka zinazohusika kuendelea kushirikiana na taasisi za kihabari kuhakikisha sheria zote zinazowakwaza wanahabari na vyombo vya habari zinafanyiwa marekebisho ili kuimarisha upatikanaji wa habari sahihi katika mazingira salama.

Awali akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), Abdallah Abrahmani Mfaume, Katibu Mkuu, wa klabu hiyo, Mwinyimvua Abdi Nzukwi, alieleza kuwa maadhimisho hayo yanafanyika kukuza na kuimarisha kada ya habari nchini.

Hivyo aliwapongeza wanahabari kwa kuendelea kufanya kazi ya kuipatia jamii habari licha ya kuwepo kwa sera na sheria zisizoendana na wakati uliopo na kuwataka kuendelea kufanya hivyo hasa wakati huu nchi ikijiandaa na uchaguzi mkuu.

“Tunajua kuwa tunafanya kazi kwenye mazingira ambayo kisera na kisheria yana changamoto lakini kwa vile bado sheria na sera hizo hazijarekebishwa tunapaswa kuishi nazo huku tukizingatia mingi ya maadili ya kazi zetu ili twe salama”, alieleza Nzukwi.   

Naye Mratibu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) ofisi ya Zanzibar, Ziada Ahmed Kilobo, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, alisema usalama wa wandishi wa habari ni muhimu hususani katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu ambapo serikali ina jukumu la kuhakikisha waandishi wa habari wanafanya kazi zao bila ya vitisho.

Aliongeza kuwa ili kuwa na jamii iliyoelimika, kunahitajika kuwa na vyombo vya habari makini na huru vinavyoweza kutoa habari na uchambuzi wa kina unaowafanya wananchi kufanya maamuzi sahihi.

Kwa upande wake,  Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar, Salum Ramadhan Shaaban, alisema changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta ya habari zipo njiani kutatuliwa ikiwemo ya kupatikana kwa sheria mpya ya habari na sera ambayo alisema imeshakamilika.

Alifafanua kuwa hatua hizo zinachukuliwa ili kuwawekea waandishi wa habari mazingira mazuri ya kazi ambapo wizara kupitia idara hiyo itashirikiana na wadau kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari kuimarisha utendaji wao.

Naye Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Dk. Mzuri Issa Ali, akiwasilisha maazimio ya kongamano hilo alisema waandishi wana wajibu wa kuandika habari kwa weledi na kuzingatia maadili hivyo wanayo haki ya kupata sheria ya habari inayolinda maslahi kama ilivyo kwa watendaji wa kada nyengine.

“Sote ni wataalamu na tunafanya kazi kwa kuzingatia hilo lakini lazima tupatiwe haki yetu ya kuwa na sheria nzuri ya habari, kufuatilia michakato ya sheria, kupewa ulinzi pamoja na kutopewa vitisho na kufanya kazi kwa usawa na ukweli”, aliongeza Dk. Mzuri.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar, Salum Ramadhan Shaaban, akizungumza wakati wa kongamano.


Mwandishi Mtangazaji wa kituo cha Redio ya Zenji FM, Berema Suleiman, akichangia mada wakati wa kongamano

Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo (WAHAMAZA), Jabir Idriss, akitoa maoni yake wakati wa kongamano.

Siku ya Uhuru wa Habari Duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo Mei 3, ambapo kwa Zanzibar kauli mbiu iliadhimishwa jumamosi iliyopita chini ya kaulimbiu ya ‘Sheria nzuri ya habari ni chachu ya uchaguzi ulio huru na wa haki’. 


Comments

Popular posts from this blog

Airtel Foundation yazindua mpango wa udhamini wa masomo kwa vijana

ZAMECO yakerwa na video ya udhalilishaji mtandaoni

SMZ yawaita vijana kushiriki kilimo