'Zanzibar Matibabu Card' yashinda tuzo ya WSIS
NA MWANDISHI MAALUM, USWISI
WIZARA ya Afya Zanzibar imetunukiwa tuzo ya kimataifa ya ‘World Summit on the Information Society’ (WSIS) kutokana na mafanikio ya utekelezaji wa mfumo wa matibabu kwa njia ya kadi maalum ya kidijitali ijulikanayo kama ‘Zanzibar Matibabu Card’, ambao umewezesha utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi kupitia teknolojia.
Hafla ya kukabidhi tuzo hiyo ilifanyika Geneva, Uswisi na kuhudhuriwa na Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa tanzania, Jerry Slaa, Balozi wa Tanzania Geneva, Abdallah Possi, pamoja na wajumbe kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao Zanzibar (e-GAZ) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Akipokea tuzo hiyo kwa niaba ya Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar, Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alisema mpango huo ni uthibitisho wa dhamira
ya taifa kutumia teknolojia kuboresha maisha ya wananchi.
Alieleza kuwa mfumo huo umeunganisha
vituo vyote vya afya vya umma na taarifa za matibabu za wagonjwa kwa njia ya
kidijitali, hatua inayochochea uwazi, ufanisi na usawa katika sekta ya afya.
“Mpango huU unawezesha upatikanaji na utoaji wa huduma za afya katika eneo lolote, ukiwa mfano wa kuigwa kwa nchi za kipato cha chini na cha kati zinazolenga kufikia mpango wa Huduma za Afya kwa wote (UHC) kupitia mifumo ya kidijitali”, alisisitiza Mazrui.
Akizungumzia hatua hiyo, Mkurugenzi wa
Programu wa PharmAccess, Faiza Abbas, alisema mradi huo umedhihirisha uwezo wa
uvumbuzi wa kidijitali katika kufanikisha huduma bora za afya na kuziba pengo
la usawa.
Alibainisha kuwa mfumo huo unaunganisha
moja kwa moja rekodi za matibabu kupitia mifumo mbalimbali kama SHAMS-EMR,
NSK-EMR na ZanEMR kwa ngazi tofauti za huduma nchini na hivyo kusaidia
usimamizi bora wa afya ya jamii.
Faiza alieleza kuwa mafanikio ya mradi
huo yamewezeshwa na ushirikiano wa karibu baina ya PharmAccess, UNICEF, ZEDCo,
NSK Tanzania na Hospitali ya Saifee.
Alisema kuwa ushirikiano huo umesaidia
kuhakikisha mfumo huo wa kidijitali unalingana na sera za taifa na
umeunganishwa na kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi (ZanID) pamoja na vyeti vya
kuzaliwa, hatua inayolenga uendelevu wa mpango huo kwa miaka mingi ijayo.
Kwa mujibu wa Faiza, Kadi ya Matibabu
Zanzibar ni mfano bora unaoonyesha namna ambavyo matumizi ya teknolojia
yanaweza kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wote na kusaidia nchi za
kipato cha chini na cha kati kufikia huduma jumuishi za afya kwa wote (UHC).
Tuzo hiyo ya WSIS imekuja wakati ambapo
serikali nyingi duniani zinatafuta mifumo ya afya yenye usawa na inayostahimili
changamoto mbalimbali.
Mpango wa ‘Zanzibar Matibabu Card’ tayari
umesajili zaidi ya wananchi milioni 1.7, huku miundombinu ya kidijitali
ikiruhusu hospitali na vituo vya afya vya jamii kushirikiana taarifa za
wagonjwa kwa wakati halisi.
Comments
Post a Comment