Vyombo vya habari vinapaswa kusimamia mshikamano wa Afrika - UAJ
NA MWANDISHI MAALUM, CAIRO
MSHAURI wa Baraza Kuu la Usimamizi wa Vyombo vya Habari nchini Misri, Reem Hindi, ameeleza haja ya vyombo vya habari barani Afrika kusimamia msingi wa mshikamano wa Kiafrika ili kustawisha maendeleo ya bara na tasnia ya habari kwa ujumla.
Alitoa rai hiyo wakati akifungua mafunzo ya 61 yaliyoandaliwa na Umoja wa Waandishi wa Habari wa Afrika (UAJ) kwa kushirikiana na Baraza Kuu la Udhibiti wa Vyombo vya Habari yanayoendelea jijini Cairo, Misri yanayoshirikisha waandishi wa habari kutoka mataifa 20 ya Afrika huku Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) ukiwakilishwa na mwanachama wa Klabu ya Waaandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), Khairat Haji Ali.
Mshauri huyo aliweka wazi dhamira ya nchi hiyo kuunga mkono jitihada za UAJ za kujenga weledi na uhuru wa vyombo vya habari barani Afrika kama miongoni mwa mikakati ya kukuza kasi ya maendeleo na demokrasia.
“Kupitia mafunzo, mijadala na kubadilishana uzoefu, vyombo vya habari vitaweza kusaidia nchi za Afrika kukua kiuchumi, kisiasa na kijamii jambo litakaloongeza kasi ya maendeleo”, alieleza Reem.
Nae Mhariri Mkuu wa gazeti la Al-Ahram Weekly na Ahram Online, Ezzat Ibrahim, aliyemwakilisha Rais wa umoja huo, Mahfouz Al-Ansary, alisisitiza kuwa mustakabali wa vyombo vya habari barani Afrika ni jukumu la Waafrika wenyewe kupitia mshikamano na ushirikiano.
Alieleza kuwa mafunzo yanashirikisha waandishi 22 wakiwemo viongozi wa vyama vya wanahabari ambapo mada kuu ya mafunzo ni nafasi ya Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), uandishi wa habari katika maeneo yenye migogoro, maadili ya taaluma na nafasi ya vyombo vya habari katika utetezi wa haki za binadamu na maendeleo ya kijamii.
“Mbali na semina, washiriki wanajifunza matumizi ya teknolojia mpya kama akili bandia (AI) katika uhariri na uzalishaji wa habari, sambamba na ziara za kitaaluma katika vyombo vikubwa vya habari na taasisi za elimu nchini Misri”, alieleza Ezzat.
Mwakilishi wa UTPC katika mafunzo hayo, Khairat alieleza kuwa uwakilishi wake sio tu unadhihirisha nafasi ya Tanzania katika meza ya mijadala ya kitaifa na kimataifa, bali pia unapanua upeo wa waandishi wa habari chipukizi na wazoefu katika kushiriki mafunzo ya kitaalamu.
“Kupitia fursa hii, UTPC inaendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuwekeza katika weledi wa wanahabari wake kama chachu ya maendeleo ya kidemokrasia na kijamii nchini Tanzania jambo linalopaswa kupongezwa na kuendelezwa”, alisisitiza Khairat.
Aidha Khairat alitoa rai kwa washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha kuwa vyombo vya habari vya nchi zao vinafikia dhamira ya kuwa daraja la mshikamano wa kiafrika, dira ya kujenga tasnia huru na yenye maadili lakini pia jukwaa la kukuza ushirikiano utakaoisaidia Afrika kuandika simulizi zake kwa sauti yake.
Nae Olivier Nakanwagi, mwandishi wa habari kutoka Uganda, alisema ni muhimu waandishi wa Afrika kuandika habari njema na sahihi kuhusu bara lao ili kuepuka upotoshaji huku akisisitiza umuhimu kuanzishwa kwa njia zetu za mawasiliano zinazozungumzia nchi za Afrika vinavyoweza kufikiwa hata na watu walio nje ya bara.
“Nadhani waandishi wa Afrika tunapaswa kuangazia zaidi ubunifu, ujasiriamali na mafanikio ya kitamaduni ili vyombo vya habari vya kimataifa vipate picha halisi ya bara letu”, alieleza Oliver.
Nae Youssef El Khaider, kutoka Morocco, alisisitiza kuwa mafunzo hayo siyo tu fursa ya kujifunza mbinu mpya za uandishi, bali ni jukwaa muhimu la mshikamano wa kitaaluma unaoimarisha sauti za waandishi wa habari katika kupigania demokrasia, haki za binadamu na maendeleo ya jamii za Afrika.
“Mafunzo haya yametupa nafasi ya kujifunza, kushirikiana na kuelewa changamoto za kila nchi. Afrika ina kila kitu isipokuwa mshikamano na nia ya dhati. Ni wajibu wetu kuunganisha nguvu, kuandika historia yetu wenyewe na kulinda amani, kwa sababu wananchi ndio huchukua gharama kubwa ya migogoro,” alisema Youssef.
Akizungumzia umuhimu wa mafunzo haya, Fanta Diakite, mwandishi wa habari kutoka Mali, alieleza kuwa mafunzo haya ni jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu na kujifunza kutoka kwa waandishi wa habari wa mataifa mbali mbali.
Alisisitiza kwamba kazi ya uandishi siyo tu kutoa taarifa, bali pia kuimarisha mshikamano na kulinda heshima ya nchi na bara la Afrika kwa ujumla hivyo waandishi wa habari wa Afrika wanapaswa kuandika kwa kuzingatia maslahi na mazingira ya nchi zao kwani sisi ndio sauti ya wananchi na sauti ya wasio na sauti.
Comments
Post a Comment