Ayoub ahimiza wazazi, walezi kushirikiana kuinua elimu
NA MWANDISHI WETU
![]() |
MKUU wa mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud |
MKUU wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud, ametoa wito huo wakati wa mahafali ya kwanza ya wananfuzi wa kidatoncha pili wa skuli ya sekondari Ghana iliyopo katika shehia ya Ghana, wilaya ya Kati mkoani humo.
Alisema ushirikiano kati ya pande mbili hizo ni nyenzo muhimu katika kutatua changamoto zinazowakabili wanafunzi pamoja na kufanikisha malengo ya
walimu ambayo ni kuongeza ufaulu wakati wa mitihani ya taifa.
Alisema, kamati ya maendeleo ya
elimu ya shehia hiyo imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha inaanza ujenzi wa
madarasa mengine mapya ili kusudi kuhamasisha wengine kuchangia ujenzi wa
madarasa hayo.
Hivyo, aliwataka wananchi kuchangia miradi ya kijamii ikiwemo ujenzi wa madarasa katika skuli hiyo na kuahidi kuwa atawashauri wamiliki wa viwanda vya kokoto,viwanda vya matofali na mashimo ya kifusi waliopo mkoani humo kuchangia ujenzi wa skuli hiyo ili iendeleze ujenzi wa madarasa hayo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya elimu katika shehia ya Ghana, Ali Mohammed Othman alisema kamati yake imefanikiwa kuongeza mwamko juu ya masuala ya elimu kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
Alisema katika skuli
yao waliweka kambi za wanafunzi wanaotarajiwa kufanya mitihani ya taifa
pamoja na kuanzisha ujenzi wa vyumba vya madarasa mapya na kuongeza nafasi za
kujisomea.
Nae mfanyabiashara, Said Nassir
Bopar, katika hatua ya kuunga mkono juhudi za serikali za kuinua sekta ya
elimu, aliahidi kuisaidia skuli hiyo mabati 150 kwa ajili ya kuezekea mabanda yaliyojengwa
kwa nguvu za wananchi.
“Sambamba na mabati hayo, pia
nitawapatia kompyuta tano ili ziongeze ufanisi kwa walimu na wanafunzi katika
mitihani yao na kazi za kila siku,” alieleza Bopar.
Asilimia 79.29 ya wanafunzi
wote wa kidato cha pili waliofanya mitihani ya taifa katika skuli hiyo, walifaulu
na kuendelea na kidato cha tatu huku skuli hiyo ikikabiliwa na changamoto za uhaba
na uchakavu wa majengo na kukosekana kwa hati miliki za maeneo ya skuli hiyo.
Comments
Post a Comment