Bodi yatakiwa kutokuwa chanzo cha migogoro
NA MWANDISHI WETU
WAJUMBE wa Bodi ya Uhaulishaji
Ardhi Zanzibar, wametakiwa kutokuwa chanzo cha migogoro ya ardhi na badala yake
kuwa watatuzi wa migogoro hiyo kuwa mujibu wa sheria zilizopo.
Akizungumza na Wajumbe bodi hiyo ofisini
kwao Forodhani, Waziri wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, Riziki Pembe
Juma, amesema kufanya hivyo kutasaidia kuondoa migogoro ambayo inaongezeka siku
hadi siku.
“Sheria zilizopo zinaelekeza mambo
yote yanayotakiwa na yasiyotakiwa kufanyiwa kazi, hivyo sio vyema kufanya kazi
kwa utashi binafsi badala yake mfanye kazi kwa mujibu wa sheria zilizopo na sio
kuwakandamiza wananchi ambao sisi ndio wanaotutegemea,” amesema Pembe.
Ameongeza kuwa ipo haja ya kukaa
pamoja kati ya wajumbe wa bodi hiyo na kamisheni ya ardhi ili kuzifanyia
mapitio na marekebisho sheria zenye mapungufu ili kuona zinakidhi mahitaji.
Nao Wajumbe wa Bodi hiyo, walisema
kuwa miongoni mwa vikwazo wanavyokabiliana navyo ni baadhi ya wananchi kuuza
maeneo kwa zaidi ya mtu mmoja hali inayopelekea kutomtambua mmiliki halali.
Wakati huo huo, Waziri Pembe, ameiagiza
Kamisheni ya Ardhi kumpatia hati halali ya umiliki wa ardhi wa ekari moja
iliyopo Jumbi, wilaya ya Kati Unguja Ali Talib baada ya kujiridhisha kuwa
mmiliki halali wa eneo hilo.
Aidha amemtaka Saleh Karama aliedaiwa
kuvamia eneo hilo na kuanzisha gereji kuhamia katika eneo jengine alilopangiwa
kihalali.
Amesema, serikali imeamua
kuyafatilia maeneo yote yenye migogoro ili kufahamu wamiliki halali na kila
mwananchi apate haki yake kisheria.
Nae, Mmiliki wa eneo hilo, Ali
Talib, ameishukuru serikali kupitia wizara hiyo kwa kummilikisha eneo hilo
ambalo analimiliki tokea mwaka 2003 na kuiomba wizara kuyapatia ufumbuzi maeneo
yote yenye migogoro ili wananchi waishi kwa amani.
Mkuu wa Kitengo cha eka na ardhi za
kilimo, Omar Ameir Pandu, amesema ni vyema wananchi kufata sheria zilizopo za
matumizi ya eka za kilimo na kuacha tabia za kuzitumia kwa shughuli za makaazi.
Ziara ya Waziri Pembe, ilikuwa na
lengo la kuangalia maeneo mbali mbali yenye migogoro ambapo alitembelea Jumbi
wilaya ya Kati, Kianga, Chuini na Kama wilaya ya Magharibi ‘A’, Unguja.
Comments
Post a Comment