Miaradi ya TASAF ikidhi viwango - Waziri

NA MWANDISHI WETU

MFUKO wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF), imetakiwa kuhakikisha ubora na viwango katika miradi ya jamii inayoanzishwa badala ya kufuata utashi wa viongozi wa kisiasa.

(Pichani ni Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Ladislaus Mwamanga (katikati) akieleza jambo alipokutana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar walipofika ofisini kwake kabla ya kukutana na waziri wa Wizara hiyo Dk. Khalid Salum Mohamed).

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratatibu na Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid Salum Mohamed, amesema uwekezaji wa TASAF katika miradi hasa ya ujenzi wa majengo ya jamii unapaswa kuzingatia viwango ili kuepusha hasara ya mali na maisha ya watu.

Akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislauds Mwamanga na ujumbe wake uliofika ofisini kwa Dk. Khalid Vuga jijini Zanzibar, hivi karibuni alieleza kuna ulazima wa miradi inayofadhiliwa na TASAF kuhakikisha kwamba inafikiwa viwango na isiwe kuwafurahisha viongozi wa majimbo.

Alisema ili miradi hiyo iwe na kiwango lazima viongozi na watendaji wa TASAF kuhakikisha wanafuata sheria na taratibu zilizopo bila ya kujali ama kuangalia maslahi binafsi ya viongozi hao.

Dk. Khalid alimuomba Mkurugenzi huyo kuwapatia taaluma wajumbe wa Baraza la wawakilishi na watendaji wengine wanaoshughulikia eneo hilo ili wapate uelewa wa lengo la TASAF pamoja na azma ya serikali.

Aidha alisema njia hiyo itasaidia kuondosha usumbufu wa kulazimisha mambo yasiyo na msingi wa malengo yaliyokusudiwa ndani ya mradi huo yatimie kwa muda uliokusudiwa.

Dk. Khalid alisema ipo haja kwa watendaji kubadilika kwa kuongeza bidii katika kazi, kuongeza umakini pamoja na kusimamia vizuri uwajibikaji kwani itasaidia kuleta mabadiliko ya haraka nchini.

Mbali na hilo waziri huyo alimshauri kiongozi huyo uanzishwe utaratibu wa kufuatilia waliomaliza kupatiwa ruzuku ndani ya mradi huo kutokana na kujikimu kimaisha ili wajiendeshe vizuri.

“Ipo haja ya kuwafuatilia kwa karibu walengwa hao hasa katika suala zima la uendeshaji wa miradi yao ili panapojitokeza changamoto wapatiwe ufumbuzi unaofaa na kwa wakati waweze kusonga mbele,” alisema.

Dk. Khalid aliishauri TASAF kufikiria kujenga kufadhili ujenzi wa dakhalia za wanafunzi katika maeneo ya vijijini ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira bora na kuongeza kiwango cha ufaulu.

Aliuahidi uongozi wa mfuko huo kwamba atashirikiana nao kwa karibu huku akifuatilia uwekezaji wa miradi ili kasoro zilizopo zitatuliwe kwa kutumia mbinu na utaalamu kuleta tija kwa walengwa. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji TASAF, Ladislaus Mwamanga, alisema fikra na mbinu za kitaalamu alizozitoa waziri huyo wakati akiwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, zimeleta mafanikio makubwa ndani ya mradi huo.

Alisema kuna mambo na mikakati ambayo Dk. Khalid alishauri inaendelea kutumiwa na imekuwa ni miongoni mwa chachu ya kufanikiwa kwa miradi mingi iliyoanzishwa nchini hasa Zanzibar.  

Alifahamisha kwamba jumla ya shilingi bilioni 21.2 zinatarajiwa kutumika kwa walengwa wa TASAF Zanzibar na kueleza kwamba msisitizo wa serikali ni kuona maeneo yote yanatoa matokeo mazuri na ya haraka.

Mwamamnga alisema, jambo la msingi ni kuhakikisha watendaji na wataalamu wote wanatumia nafasi yao katika kuhakikisha miradi inayoekezwa inaleta tija kwa jamii nzima.

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango