Tumejipanga kuzikabili changamoto za wakulima wa mwani - Waziri
NA MWANDISHI WETU, PEMBA
IMEELEZWA kuwa mashirikiano ya wadau mbali mbali na serikali yatachochea
kasi ya kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wakulima wa mwani na zao
hilo kwa ujumla.
Akifungua mafunzo ya wakufunzi wa wakulima wa mwani katika ukumbi wa Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC), Wawi Pemba, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Dk. Soud Nahoda Hassan, alieleza kuwa kupitia dhana ya uchumi wa bluu zao hilo litaimarishwa ili kuongeza uzalishaji.
“Juhudi zote hizo zinafanyika ili kuinua kipato na hali za wakulima,
hivyo niwatie moyo serikali itaendelea kushirikiana na wadau kama REPOA
(Taasisi ya Utafiti wa Sera na Maendeleo na Umaskini Afrika) katika kufikia
malengo,” alisema Nahoda.
Aidha dk. Nahoda alieleza kuwa mipango ya serikali kujenga kiwanda cha
kusarifu zao hilo itasaidia kutanua soko na kuongeza bei ya zao hilo jambo
litakalokuza uchumi wa wakulima hao na Zanzibar kwa ujumla.
“Mahitaji ya kiwanda kinachojengwa ni tani 30,000 wakati uzalishaji kwa sasa ni chini ya tani 20,000 kwa mwaka hivyo ipo haja ya kutafuta mbinu za kuongeza uzalishaji utakaokidhi mahitaji ya kiwanda lakini pia kusafirisha nje,” aliongeza Dk. Nahoda.
Washiriki wa mafunzo ya wakufunzi wa wakulima wa mwani wakifuatilia mafunzo.
Awali akitoa taarifa kuhusiana na mafunzo hayo, katibu mkuu wa wizara ya biashara na maendeleo ya viwanda, Juma Hassan Reli, alisema yamelenga kuwajengea uwezo wakulima kuzalisha mwani katika maji makubwa kinyume na ilivyo sasa.
Alisema katika mafunzo hayo wakufunzi hao ambao wanatoka katika maeneo
mbali mbali ya kisiwa cha pemba, watapatiwa mbinu za uzalishaji na namna ya
kujikinga na madhara yanayotokana na uzalishaji wa mazao hayo.
Aidha aliongeza kuwa, pamoja na mafunzo, wizara yakle imeandaa sera ya
mwani ambayo imelenga kuimarisha uzalishaji, kuongeza thamani na bei ya zao
hilo.
“Kwa sasa ZSTC (Shirika la Biashara la Taifa) linanua mwani wa cotonee
kwa shilingi 1,800 kwa kilo hivyo kupitia mafunzo haya tunaamini uzalishaji
utaongezeka na kupata ziada ya tani 12,000 ambazo zitauzwa kwa wanunuzi
wengine,” alieleza Reli.
Aliongeza kuwa hatua hiyo inawahakikishia wakulima wa mwani soko la
uhakika na kuishukuru REPOA kwa kufanya tafiti za maendeleo ya zao hilo lakini
pia kuwajengea uwezo wakulima na wadau wengine wa zao hilo kukuza uchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari kando ya mafunzo hayo, Waziri Mstaafu
wa Biashara na Viwanda, Balozi Amina Slaum Ali, aliipongeza serikali ya awamu
ya nane kwa kuendeleza programu za maendeleo ya sekta ya mwani ambayo alisema
imekuwa na mchango mkubwa kwa wananchi hasa wanawake.
Viongozi wa meza kuu wakiongozwa na Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo (wa tatu kutoka kulia) Soud Nahoda Hassan wakiwa katika mafunzo hayo. Wa kwanza ni Balozi Amina Salum Ali, Waziri Msataafu wa Biashara na Viwanda.
“Kwa muda mrefu kilimo cha mwani kinafanywa na wanawake, wakati umefika kwa vijana wakiume na wananume kushiriki katika kilimo hiki na kuchangamkia fursa zinazopatikana kwani soko lipo na serikasali ipo tayari kusaidia,” alisema Balozi Amina.
Akitoa shukrani kwa niaba ya washiriki wengine wa mafunzo hayo, mkulima
fatma Muhammad makame wa makangale, aliishukuru serikali na wadau mbali mbali
kwa kuwapatia mafunzo hayo na mengine ambayo yamewawezesha kujikwamua kiuchumi.
“Mafunzo ya mara kwa mara yametujengea uwezo wa kusarifu mwani na
kuzalisha bidhaa za chakula na matumizi ya nyumbani badala ya kuuza kama ulivyo
kwa wafanyabiashara ambako bei ilikuwa sio nzuri sana,” alisema mkulima huyo.
Mafunzo hayo ya siku saba yatafanyika kwa nadharia na vitendo ambapo
wakufunzi hao watajifunza njia mbali mbali za uzalishaji wa mwani katika maji
makubwa, namna bora ya utunzaji na kuliongezea thamani zao hilo.
Baada ya kufungua mafunzo hayo, Dk. Nahoda akiambatana na maafisa wa
taasisi ya REPOA walitembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya kiwanda cha
kusarifu mwani liliopo Chamanangwe, wilaya ya Wete, mkoa wa Kaskazini
Pemba.
Comments
Post a Comment