Waandishi watakiwa kutumia fursa kujiendeleza
NA ASYA HASSAN
WAANDISHI wa habari nchini
wamesisitizwa kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa ili kuwajengea uwezo,
uelewa, kujitangaza ili kuongeza ufanishi katika kazi zao na maendeleo ya taifa
kwa ujumla.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa
klabu ya waandishi wa habari zanzibar (ZPC), Abdallah Abdulrahman Mfaume,
alipokuwa akizungumza katika kikao cha pamoja cha wanachama na viongozi wa
jumuiya hiyo kilichofanyika katika ofisi za klabu hiyo Kijangwani mjini Unguja.
Mfaume aliwasisitiza waandishi
kutumia kalamu zao vizuri pamoja na kufuata sheria na maadili ya kazi zao ili
kukuza ustawi wa jamii na kutunza amani iliyopo.
Alisema uandishi wa habari ni kada
inayotegemewa kuchochea mabadiliko na maendeleo katika jamii hivyo waandishi
wanapaswa kutambua wajibu wa kutunza amani na kutokuwa chanzo cha kuivuruga na
kuisababisha nchi kuingia katika migogoro.
“Wakati tulionao waandishi
tunatakiwa kujibiisha na kujifunza kila mara ili tuweze kuielimisha jamii,
kuiasa na kuhimiza jamii juu ya mambo mbali mbali yanayowahushu hasa amani na
utulivu,” alisema Mfaume.
Aidha Mwenyekiti huyo aliwataka
wananchama hao kuacha tabia ya kukatishana tamaa, badala yake washirikiana na
kusaidiana ili kuinya fani hiyo kuendelea kuwa na hadhi lakini pia tija kwa
jamii nzima.
Awali Katibu Mkuu wa ZPC,
Mwinyimvua Abdi Nzukwi aliwapongeza waandishi hao kwa kujitokeza na kutumia
fursa mbalimbali zinazojitikeza ili zileta tija kwao na taifa kwa ujumla.
Alisema ni vyema kwa kila mwandishi
akachangamkia fursa hizo kwani zinatoa nafasi ya kukukuza ujuzi wao lakini pia
kusaidia jamii.
Alisema kupitia umoja wao, fursa
nyingi hujitokeza hivyo ni vyema kwa waandishi kuzitumia kwa namna moja au
nyengine kwani zinawasaidia kujitangaza na kuleta mabadiliko katika kutekeleza
majukumu yao.
Alizitaja baadhi ya fursa hizo kuwa
pamoja na mafunzo kwa wandishi wa habari na mashindano yanayolenga kuongeza
uelewa wa jamii juu ya mambo mbali mbali lakini pia kujenga uwezo wa mwandishi
binafsi.
“Mnaweza kuona mmefanya jambo la
kawaida, lakini kazi za uandishi mlizozitoa kwenye vyombo vyenu zimekuwa na
mchango mkubwa katika mabadiliko ya jamii yetu, tuendelee kuzifanya hata baada
ya hapa,” alisisitiza Nzukwi.
Aidha Katibu huyo alitumia fursa
hiyo kutambulisha mradi wa ujenzi wa amani, uvumilivu wa kisiasa na uwezo wa
jamii kupokea tofauti za maoni unaofadhiliwa na shirika la internews na kuwaomba
waandishi wa habari kuendelea kuandika habari zitakazoimarisha umoja miongoni
mwa jamii.
Wakizungumza katika kikao hicho,
wanachama hao waliomba viongozi hao kuendelea kutafuta fursa za mafuno kwa
waandishi wa habari ili kuimarisha utendaji wao kulingana na wakati uliopo.
Walieleza kuwa, uandishi wa habari
za magonjwa ya miripuko ikiwemo covid 19, umewapa nafasi ya kujua zaidi kuhusu
maradhi hayo.
“Tunawashukuru kwa fursa hii lakini
tunawaomba viongozi muendelee kutusaidia kwa kutuunganisha katika fursa mbali
mbali zinazotokezea ili tuzidi kujielimisha, kujitangaza na kuongeza kipato”,
alieleza mmoja ya wanachama hao.
Kikao hicho kilichofuatiwa na kikao
cha kamati tendaji cha klabu hiyo, kilipitia kazi zilizofanywa na waandishi hao
kupitia mpango wa kujenga uelewa wa jamii juu ya maradhi ya miripuko
uliofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA) unaosimamiwa na Muungano
wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).
Comments
Post a Comment