Wadau wataka mjadala kuweka misingi ya amani

NA MWAJUMA JUMA

WADAU wa amani na uchaguzi nchini wameishauri na wadau wengine wa uchaguzi kuitisha mjadala wa pamoja utakaotoa suluhuhisho la hofu ya kuvunjika kwa amani kipindi cha uchaguzi.

Wakizungumza katika mkutano  ulioitishwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), walisema pamoja na Zanzibar kuendelea kuwa na amani baada ya uchaguzi wa oktoba mwaka huu, ipo haja ya kutafutwa mbinu zitakazoondoa hofu ya kuondoka kwake kila ifikapo wakati wa uchaguzi.

Mkurugenzi wa Jumuiya ya Vijana na Maendeleo Zanzibar (ZAFAYCO), Abdallah Abeid, alieleza kuwa ili kuimarisha misingi ya amani iliyopo, kuna haja ya wadau kushirikiana na serikali kutafuta kiini cha hofu ya kuvunjia amani kila inapokaribia kipindi hicho.

“Imezoeleka kila inapotokea uchaguzi, hofu juu ya kuvunjika kwa amani inaongezeka hivyi ipo haja ya kutafuta chanzo cha hiyo hofu na kuiondoa,” alisema Abeid.

Nae Maryam Chum alieleza kuwa kuna umuhi kwa jamii kueleweshwa mbinu za kukabiliana na viashiria vya uvunjifu wa amani ili kuzuia madhara ambayo huwaathiri zaidi wanawake na watoto.

Maryam ambae ni mjumbe wa chama cha wanahabari wanawake Tanzania (TAMWA) ofisi ya Zanzibar alisema, inapotokea machafuo katika jamii, vitendo vya udhalilishaji na ukatili dhidi ya makundi hayo huongezeka.

“Siku za nyuma tumeshuhudia mambo haya lakini hata katika hiki kipindi cha amani, ukatili dhidi ya wanawake umeripotiwa kwa baadhi ya wanawake kupewa talaka kwa kutotekeleza matakwa ya waume zao,” alieleza Maryam.

Maryam Chum kutoka TAMWA ofisi ya Zanzibar akichangia katika mkutano huo.

Kwa upande wake Afisa Mipango wa ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar Abdul-latif Moh’d, alieleza kuridhishwa kwake na jinsi vyombo vya habari vilivyohamasisha jamii kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani wakati wa uchaguzi.

“Kwa uchaguzi uliopita, kila mdau alichukua nafasi yake kwani hata ofisi yetu ilitoa mwongozo kwa Maimamu na Masheikh kuhakikisha wanahubiri amani katika misikiti,” alisema Abdul-latif.


Afisa Mipango katika Ofisi ya Mufti Mkuu Abdul-latif Mohamed akitoa maoni yake katika mkutano huo.

Nae Mchungaji wa kanisa Anglican Zanzibar, Father Philip Munguti aliongeza kuwa, misingi ya amani inapaswa kujengwa katika ngazi ya familia na mtu mmoja mmoja.

“Amani ni tunda la haki lakini chanzo kikuu cha amani ni nafsi ya mtu na ndio maana sisi (kanisa) tunawahubiria waumini wetu juu ya jambo hilo ili kupata jamii yenye kuheshimu amani ya wengine,” alieleza Father Munguti ambae pia aliipongeza ZPC kwa kuitisha mkutano huo.

Father Philip Munguti wa Kanisa Anglican Zanzibar akichangia mada.

Aidha Mkuu wa usalama barabarani (RTO) wa mkoa wa Mjini Magharibi, ASP Issa Ahmad Mlanzi, alieleza kuwa jeshi la polisi licha ya kuwa na dhima ya kuwalinda raia na mali zao, linahitaji ushiriki wa jamii ili kustawisha amani na utulivu ndani ya jamii.

“Siku zote polisi wapo katika jukumu la kulinda amani iwe ndani au nje ya uchaguzi, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha amani yake na raia mwenzake inakuwepo, hilo linawezekana iwapo vikao kama hivi vitafanyika mara kwa mara,” alieleza ASP Milanzi aliyemuwakilisha Kamanda wa polisi wa mkoa huo katika mkutano huo.

ASP Milanzi akitoa maoni yake. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa ZAFAYCO Abdallah Abeid.

Mapema akiwasilisha mada, mhadhiri wa skuli ya uandishi wa habari na mawasiliano ya umma ya Chuo kikuu cha taifa Zanzibar (SUZA) Dk. Aboubakar Rajab, alieleza umuhimu wa wadau wa uchaguzi kujadiliana namna wanavyoweza kuwaunganisha wananchi na wanachama wa vyama vyao ili kuimarisha amani na usalama wa nchi.

“Pamoja na mgawanyiko kuwa chanzo cha mapatano, maafikiano na kuimarisha utengamano katika jamii, bado ipo haja ya kuwarudisha pamoja wananchi ambao wamegawanyika kutokana na matokeo ya uchaguzi toka ndani ya vyama hadi katika uchaguzi wa taifa,” alieleza Dk. Aboubakar.

Alisema jamii inapaswa kutambua kuwa amani sio kitu cha kudumu na kinachopaswa kkulindwa ili kisitoweke kwani ikitokea hivyo kuna gharama kubwa kuirudisha.


Dk. Aboubakar Rajab (wa pili kushoto) akifafanua jambo katika mkutano huo.

Mkutano huo wa siku moja, ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa amani, uvumilivu wa kisiasa na utamaduni wa kupokea maoni tofauti kabla, wakati na baada ya uchaguzi, unaotekelezwa na ZPC kwa ufadhili wa shirika la Internews kupitia mpango wa Boresha Habari.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango