Wanahabari endelezeni uzalendo, kuhamasisha amani – RC Kitwana
NA ASYA
HASSAN
MKUU wa
Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa, amesema vyombo vya habari vina
wajibu mkubwa wa kuendelea kushajiisha jamii juu kuongeza mshikamano, kutunza
amani na kuvumiliana.
MKUU wa mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana akifungua semina hiyo. Kushoto ni Mwenyekiti wa ZPC, Abdalla Mfaume.
Ameeleza hayo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kuandika habari zinazohamasisha amani, umoja, mshikamano na mtangamano wa kijamii baada ya uchaguzi yaliyofanyika Kidongo Chekundu, Zanzibar.
Mafunzo
hayo yaliyoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC) kwa
kushirikiana na Shirika la Internews Tanzania, ni sehemu ya utekelezaji wa
mradi wa kukuza amani katika jamii.
Waandishi wa habari wanachama wa ZPC wakiwa katika mafunzo ya uandishi wa kuhamasisha amani.
Alisema
amani, umoja na mshikamano ni muhimu katika nchi yoyote kwani ndio msingi wa
maendeleo na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Alisema,
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi,
anasisitiza amani, utulivu na mshikamano wa jamii katika kujenga nchi yenye
maendeleo, hivyo vyombo vya habari vinapaswa kuandaa habari na vipindi
vitakavyoimarisha umoja na mshikamano wa wazanzibari badala ya kuwagawa.
"Hakuna
kitu muhimu na chenye thamani zaidi ya uzanzibari na umoja wetu, kwani huo ndio
msingi imara utakaochochea kasi ya maendeleo ya nchi yetu,” alisema.
Waandishi wa habari, wanachama wa ZPC wakifuatilia uwasilishaji mada katika mafunzo ya uandishi wa kuhamasisha amani.
Alisema nchi isiyokuwa na amani haiwezi kupata maendeleo, hivyo ni lazima amani iwepo kwa kila kundi katika jamii.
Akitolea
mfano wa nchi zilizoingia katika machafuko, Kitwana alisema zimeingia katika
migogoro kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo uchochezi uliofanywa na
waandishi wa habari, hivyo aliwataka waandishi wa habari kujifunza makosa ya
wenzao.
Aliwapongeza
waandishi wa habari kwa kazi kubwa waliyoifanya wakati wa uchaguzi mkuu kwa
kutoa taarifa ambazo zilichangia kupatikana kwa amani na upendo miongoni mwa
jamii.
"Dhima hii ni yetu sote na mlifanya kazi hii kwa kuamini kwamba nanyi mnahusika katika ujenzi wa amani kwani kazi hii ilikuwa tuifanye sisi viongozi wa siasa katika majukwaa yetu,” alisema.
Aidha
aliishukuru ZPC kwa kuandaa mafunzo hayo na kuwashajiisha wanachama wake kuona
umuhimu wa kuhamasisha amani, utulivu na mshikamano wa kijamii katika maeneo
yao.
"Naamini
kama mtatumia kalamu zenu na midomo yenu vizuri na kuongeza hamasa ya kuwaona ya
kuhakikisha wazanzibari wanabaki katika hali ya amani na utulivu, bila shaka
mtakuwa mnathibitisha uzalendo wenu," alisema.
Akizungumzia
ushirikiano kati ya ofisi yake na waandishi wa habari, aliwasisitiza watumishi
walio chini yake kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari wanapokwenda kufuata
taarifa kwao.
Alisema
mtumishi yeyote ambaye hatotoa ushirikiano kwa wandishi wa habari na kuficha
taarifa atashughulikiwa.
Aliwashauri
Wanahabari na vyombo vya habari kuibua changamoto zinazotokea katika jamii kwa
lengo la kuisaidia serikali ya awamu ya nane kufikia malengo yake.
Mapema
Mwenyekiti wa ZPC, Abdalla Abdulrahman Mfaume, alisema mafunzo hayo
yanayofadhiliwa na shirika la Internews ni muhimu katika ujenzi wa jamii yenye
mshikamano na umoja.
Hata hivyo, aliwahimiza wanapoandika habari zao wasipuuze mawazo mbada kutoka makundi mengine katika jamii.
MWANDISHI wa habari mwMWANDISHI wa habari mwandamizi Ali Sultan (aliesimama) akiwasilisha mada ya maadili ya uandishi wa habari na uandishi wa habari za amani (peace journalism).Katika
mafunzo hayo ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kujenga amani, uvumilivu wa kisiasa na utamaduni wa kupokea maoni tofauti unaotekelezwa na ZPC kwa ufadhili wa Internews, mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo ya wajibu wa vyombo vya habari katika
kudumisha amani na umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi.
Comments
Post a Comment