Soraga aitaka ZBS kuzingatia
maslahi ya umma, kudhiti ubora
NA MWAJUMA JUMA
KAIMU Waziri wa Biashara na
Maendeleo ya Viwanda, Mudrik Ramadhan Soraga, (pichani) amewataka watendaji wa Taasisi ya
Viwango Zanzibar (ZBS), kuweka mbele maslahi ya nchi wanapofanya ukaguzi wa bidhaa
na kuacha mapatano na
wafanyabiashara kwa bidhaa zisizokuwa
haina ubora.
Akizungumza na watendaji wa taasisi
hiyo iliyopo Amani viwanda vidogo vidogo alisema kuwa ZBS ni taasisi inayosimamia
viwango na watendaji wake wanapaswa kuwa makini na kutambua kuwa wanapaswa kuwa
mstari wa mbele kulinda afya za wananchi na mazingira.
“Katika hali ya kawaida nchi ya
kisiwa inakuwa kama chambo kwa kuingizwa kila kitu, ikiwa bidhaa zinaingizwa
pasi na kufuata utaratibu matokeo yake utakuta bidhaa hatarishi kwa afya za
watu zinazagaa mitaani,” alieleza.
Soraga ambae pia ni Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Kazi, Uwekezaji na Uchumi, alisema kuna baadhi ya wafanyabiashara
wanaingiza bidhaa ambazo hazina viwango hivyo ipo haja kuhakikisha wanakuwa wakali
katika usimamizi maeneo yao ya kazi.
“Tusije tukashawishika tukaacha
uzalendo wetu nyuma kwa sababu tu mtu ametoa shilingi mbili tatu, tutakua
hatuwatendei haki wananchi wetu ambao sisi kama watoa huduma wametuamini kwamba
ndio walinzi wao,” alisema.
Alisema kuwa katika kuona umuhimu
huo ameona ni vyema akakutana na watendaji hao kuwasikiliza ili kuhakikisha
bidhaa zinazoingizwa nchini zinakidhi viwango na salama kwa matumizi ya
binadamu na rafiki kwa mazingira.
Aidha alieleza kuwa ana imani na
wafanyakazi wa ZBS na kwamba wanatambua jukumu lao la kuhakikisha kwamba
wanalinda na bidhaa ambazo zinaingizwa zinakuwa na viwango bora kwa afya za
wananchi ambao wamewaamini sana.
Aidha alitaka ufafanuzi juu ya viwango
kwa bidhaa zilizotumika kwa vifaa vya umeme vinavyoingizwa nchini kwa wingi
hasa zile ambazo zimepigwa marufuku tangu 1998.
Hata hivyo alisema kuwa licha ya
kuwa na changamoto lakini wamekuwa wakitekeleza vyema majukumu yao na wao kama
Serikali watahakikisha wanaweka vitendea kazi ili waweze kufanya Kazi kwa ufanisi.
Alisema vifaa vya maabara hasa vya
‘microbiology’ ni muhimu kwa sababu kutegemea mtu wa pili katika upasishaji
sio mzuri kwani wanatakiwa wazisimamie wenyewe hasa kwa vile huwezi kujuwa huko
unakopeleka na mtu anaetakiwa ahakikiwe anaukaribu gani na huko.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa ZBS, Rahima
Ali Bakari, alisema tasisi hiyo ina changamoto kadhaa ikiwemo ya kutokuwepo kwa
mfumo wa ukaguzi bandarini utakaoiwezesha taasisi hiyo kujua mapema bidhaa
zinazoingizwa ili kuzifanyia ukaguzi kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini.
Alisema kuwa mfumo ambao upo kwa
sasa sio shirikishi na watendaji wa Shirika hilo wamekuwa wakiifanya taasisi
yao kuwa ni ya mwisho wakati wao ZBS wanatakiwa kuwa wa mwanzo kujuwa kabla ya
bidhaa kuweza kutolewa.
Aliitaja changamoto nyengine kuwa
ni kutokuwa na fursa ya kufanya ukaguzi katika maeneo ya uwanja wa ndege
kutokana na kutokuwepo kwa eneo licha ya kufuatilia upatikanaji wa eneo hilo bila
ya mafanikio.
Aidha alisema kuwa Idara ya
maendeleo ya viwango wameshakuwa na viwango 328 ambavyo vimeshatangazwa kuwa na
viwango 29 vilivikabidhiwa kwa Waziri wa biashara na viwanda ya awamu ya saba
kwa kutangaza ambapo kukamilika kwake kutaifanya Zanzibar kuwa na viwango 357
ikiwemi ni viwango vya chakula na kilimo, kemikali, uhandisi mitambo na viwango
vya mazingira.
Comments
Post a Comment