SMZ itaendelea kuwatunza wazee - Dk. Mwinyi


NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema serikali ya awamu ya nane itaendelea kutunga sera, sheria na kubuni mipango yenye lengo la kuimarisha ustawi wa wazee. 

Dk. Mwinyi alieleza hayo jana wakati akifungua semina ya mapitio ya utekelezaji wa mradi wa uwajibikaji na utimilifu kwa wazee (AFFORD II) kwa kipindi cha mwaka 2020 na mpango wa mwaka 2021, iliyofanyika katika hoteli ya Verde. 

Alisema kuwa serikali itazingatia mahitaji ya wazee katika ujenzi wa miundombinu, maakazi, pamoja na sekta ya afya na kwamba itaendelea kuimarisha ushirikiano ili jitihada za kuwatunza wazee zinapata ufanisi.

Alifahamisha kuwa ipo sheria ya masuala ya Wazee Namba 2 ya mwaka 2020 ambayo imeweka utaratibu wa upatikanaji wa haki na huduma za ustawi kwa wazee, ikiwemo urasimishaji wa mpango wa Pensheni jamii. 

Aliongeza kuwa hatua inayofuata ni kuhakikisha uundwaji wa kanuni za sheria hiyo ili iweze kutumika rasmi na kuiagiza wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Zanzibar iharakishe uundwaji wa kanuni.

Dk. Mwinyi alisema kuwa miongoni mwa mambo atakayoyapata msukumo zaidi ni pamoja na kuhakikisha kwamba kinga jamii kwa wazee inaimarishwa.

Alifahamisha kwamba serikali itaendelea kuimarisha afya za wazee nchini kwa kuhakikisha wanaendelea kupata huduma stahiki zikiwemo, huduma za afya bure na kupatiwa vitambulisho.

Alikubali ushauri wa wazee wa kuwekwa sehemu maalum kwa ajili yao kwa kupata kipaumbele cha kuhudumiwa wanapofika hospitalini kama walivyomuomba mnamo Januari 7, 2021 alipokutana nao ikulu.

Akizungumza juu ya kuongeza kiwango cha fedha na kupunguza umri wa kuanza kupata pensheni kuanzia miaka 65, Dk. Mwinyi alisema kuwa amepokea maombi hayo na ameahidi kuyatekeleza pale hali ya kiuchumi itakapoimarika.

Alisema kwamba serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha kinga jamii inapewa umuhimu katika mikakati ya kitaifa ambapo katika mpango wa miaka mitano, Zanzibar inaahidi kuendelea kurekebisha na kuimarisha mfumo wake wa kinga jamii kwa makundi yote.

Alifahamisha kwamba suala la kuwajali na kuwaenzi wazee kivitendo hapa Zanzibar ni la kihistoria ambapo licha ya kwamba mila na silka zinafunza hivyo,  lakini serikali tangu awamu ya kwanza baada ya Mapinduzi 1964 ilianza kuwahifadhi wazee kwa kuwapatia huduma za msingi.

Kwa upande wake, Kaimu Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Simai Mohamed Said, alisema uamuzi wa kufanyika mkutano huo hapa Zanzibar haukuja kwa bahati nasibu isipokuwa ni kutokana na hadhi iliyonayo Zanzibar duniani katika kuwajali, kuwaenzi na kuwaheshimu wazee.

Naye Naibu Balozi wa Ireland nchini, Chloe Horne alisema kuwa nchi yake kupitia shirika la “Irish Aid’ inaunga mkono juhudi zinazochukuliwa kuwahifadhi wazee. 

Alisisitiza kwamba nchi yake itaendelea kuratibu miradi hiyo kwa Tanzania pamoja na nchi nyengine zikiwemo Malawi, Msumbiji na Ethiopia  ambazo wamekuwa wakiziunga mkono kwa miaka 10. 

Mapema Mkurugenzi wa 'Help Age International', Smart Daniel,  alisema dunia ina wazee milioni 901 sawa na asilimia  12 ya watu wote duniani idadi ambayo ni kubwa kuliko watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na ifikapo mwaka 2050 kutakuwa na wazee  Bilioni 2.92 sawa na asilimia 21 ya watu wote duniani.

Alisema kuwa ongezeko hilo linatoa msukumo kwa dunia kutoa sera bora zaidi za kuwahudumia wazee ili  waendelee kutoa mchango wa kutukuka kwa maendeleo ya jamii zao.

Katika mkutano huo Salum Mohamed, aliwasilisha mada ya mifumo ya Ulinzi wa Jamii barani Afrika kwa kupitia mifano ya mfumo wa Kinga ya Jamii Zanzibar ambapo viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa, dini na serikali walihudhuria yakiwemo makundi ya wazee kutoka nchi za Ethiopia, Msumbiji na  Malawi.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango