Soraga awataka wajasiriamali kujengeana uwezo kibiashara
NA MWAMDISHI WETU
WAJASIRIAMALI wadogo wadogo na
wafanyabiashara wametakiwa kutumia matamasha ya kibiashara kujengeana uwezo,
umoja na kupeana taarifa zitakazoimarisha biashara nchini.
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi,
Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga ambae pia ni Kaimu waziri wa
Biashara na maendeleo ya Viwanda, alieleza hayo alipokuwa akifunga tamsha la saba
la biashara katika viwanja vya Maisara Suleiman, mjini Unguja.
Alisema iwapo wadau wa biashara
wataendelea kuunga mkono matamasha hayo, mipango ya serikali kuwawezesha
kutangaza biashara zao utafanikiwa na kuleta tija kwa jamii nzima.
Alieleza wizara yake ina mpango wa kuweka
tamasha hilo mara mbili kwa mwaka ili kutanua wigo kwa wajasiriamali,
wafanyabiashara na taasisi za umma pamoja na binafsi kutangaza biashara na
huduma wanazozitoa kwa jamii.
Alisema kuwa wizara imefarajika na
kupata matumaini makubwa kuona wanaendelea kushiriki katika maonyesho jambo
alilosema litaendelea kuungwa mkono na wizara hiyo kufanikisha matamasha kama
hayo.
“Nitumie fursa hii pia kuwaomba kusajili
biashara na shughuli zenu kwa kutumia mifumo ya kidigitali iliyopo ili muweze kutambulika
kisheria na kurahisisha ulipaji wa kodi ya serikali,” alieleza Soraga.
Aidha Waziri huyo alirejea wito wa
kuwaomba wawekezaji kujitokeza na kuwekeza Zanzibar kwani Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kupunguza kodi kwa wawekezaji
na wafanyabiashara wa bidhaa wanazozalisha au kuzileta nchini.
Akimkaribisha Waziri huyo, Katibu
Mkuu, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Juma Hassan Reli, alisema
kuwa tamasha hilo limefana kutokana na ushirikiano wa wafanyabiashara na
waandishi wa habari ambao wamelitangaza tamasha hilo lililofunguliwa na Makamu
wa rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
“Tamasha hili limefanikiwa kwa zaidi
ya asilimia 90 ambapo limewakutanisha wafanyabiashara mbalimbali pamoja na
wanunuzi sambamba na kuwajengea uzoefu wafanyabiashara na mauzo yameongezeka.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya
ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Wakulima, Hamad Hamad, alisema nia njema ya
serikali kwa wafanyabiashara kutaka kuwakuza wafanyabiashara hivyo waliahidi kuiunga
mkono serikali ili kufanya kazi zao ipasavyo.
“Jambo la busara kuwekwa kwa
wajasiriamali mbalimbali kwani wanaweza kubadilishana uzoefu wa biashara hizo
kuweza kuwa na kiwango cha juu na kuweza kuuzika katika soko la ndani na nje ya
nchi,” alieleza Hamad.
Nao baadhi ya washiriki wa maonyesho
hayo, walieleza kuwa yamewapa nafasi ya kutangaza biashara na shughuli
wanazozifanya jambo ambalo limeongeza ufanisi wa kibiashara.
Meneja wa Benki ya NMB kanda ya
Zanzibar, Abdallah Duchi, alisema benki hiyo inawathamini wajasiriamali na
wafanyabiashara wadogo wadogo hivyo itaendelea kuunga mkono jitihada zao
wanazozifanya.
“Tumejipanga kutoa suluhisho la
huduma za kifedha, kwa kuwa na mfumo bora zaidi wa ubadilishaji fedha na
biashara ya kadi,” alieleza Duchi.
Aidha Duchi aliishukuru Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwaonesha fursa kupitia kwenye uchumi wa buluu,
ambapo NMB wamekuwa na uzoefu wa biashara hizo.
Naye Meneja wa Zanzibar Cable
Televisheni, Hafidh Kassim, aliahidi kushiriki kadri itakavyowezekana katika
tamasha hilo ili iwe ni moja ya kuendelea kuwapatia wananchi habari kupitia
vyombo vyao vya habari.
Katika tamasha hilo washiriki zaidi
ya 360 wameshiriki katika tamasha hilo lililoanza Januari 5 hadi 15 mwaka huu
ambalo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 57 ya mapinduzi ya Zanzibar
yaliyofikia kilele chake Januari 12, mwaka huu katika viwanja vya Mnazi Mmoja.
Comments
Post a Comment