Waziri ataja mikakati kukuza uchumi wa bluu

NA MWANDISHI WETU

WIZARA ya Uchumi wa Bluu na Maendeleo ya imeeleza kuwa inaandaa mikatati mahsusi kukabiliana na changamoto ya uchache wa wataalamu kuzihudumia sekta zilizomo katika wizara hiyo.

Waziri wa wizara hiyo Abdalla Hussein Kombo, alisema hivi karibuni wakati akifungua kongamano lililoshirikisha wadau mbali mbali wa maendeleo katika viwanja vya Maisara. 

Alisema tatizo hilo linazikabili nchi nyingi zinazopakana na bahari, hivyo kuna haja ya kuwekwa mikakati itakayomarisha uchumi kupitia sekta mbali mbali ikiwemo ya uvuvi.

Alisema ili kufikia azma ya Zanzibar kunufaika na uchumi wa buluu, lazima sekta hiyo isimamiwe vyema na kuwekwa mkazo katika vipaumbele vya serikali ya awamu ya nane.

"Dhana ya uchumi wa bluu ni mtambuka na inahitaji ushiriki wa kila mmoja wetu, ninawaomba tuendelee kuimarisha mashirikiano baina ya serikali na sekta binafsi sambamba na wadau wengine wa maendelo," alieleza Kombo.

Aliongeza kuwa dhana ya uchumi wa bluu inajumuisha sekta nyingi za uchumi ikiwemo ya uvuvi, ufugaji wa baharini, ufugaji wa samaki, ujenzi wa viwanda vya kusindika samaki, ukulima wa mwani, bandari, usafiri na usafirishaji baharini.

"Pamoja na hayo pia, suala la utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia baharini pia ni miongoni mwa mambo yanayofungamana na uchumi wa bluu hivyo sisi kama serikali tumeamua kujikita katika maeneo hayo ili kufikia malengo ya kuimarisha uchumi wa mtu mmoa mmoja na nchi kwa ujumla,” alieleza Kombo na kuhimiza haja wananchi kudumisha amani na utulivu.

Waziri Kombo alisema changamoto hizo iwapo zitafanyiwa kazi kimkakati, uchumi wa buluu utakuwa na tija kwa Zanzibar na watu wake na kuelekeza mbinu za utekelezaji ikiwemo ya kuzifanyia mapitio sera na sheria zilizopitwa na wakati sambamba na kuwekwa mpango mzuri wa matumizi ya bahari (Special planning).

“Hatuwezi kuwa na uchumi wa buluu tukaitumia bahari kama shamba la bibi, lazima tuwe na mpango madhubuti utaonyesha namna gani tutakuwa na nia ya kuitumia bahari yetu,” alisisitiza.

Akiwasilisha madaya uchumi wa bluu, Saleh Saad Mohammed, kutoka Tume ya Mipango Zanzibar alisema, kupitia dhana hiyo fursa zitaibuliwa na kuimarisha uchumi wa Zanzibar na watu wake.

"Miongoni mwa fursa hizo ni pamoja na ujenzi wa bandari ya uvuvi baina ya serikali na sekta binafsi, ujenza wa sehemu ya kuhifadhia samaki na kujenga kiwanda cha uzalishaji barafu itakayotumika kuhifadhia samaki na mazao mengine ya baharini," alieleza Mohammed.

Nae Mkurugenzi kutoka Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu Tanzania Dk. Islam Seif Omar, alisema wakati umefika sasa Watanzania kuvua katika bahari kuu ili kujiongezea tija na faida.

"Zanzibar ina rasilimali kubwa ya wavuvi wadogo wadogo wenye ujuzi lakini wanakosa mbinu na uwezo wa kufika katika maji makubwa hivyo watakapowezeshwa pamoja na kujengewa uwezo, watavua katika bahari kuu na kuongeza kipato chao," alisema Dk. Islam.

Kongamano hilo lilihusisha wadau kutoka sekta mbali mbali wakiwemo wakulima wa mwani na wajasiamali wanaozalisha bidhaa zinazotokana na mazao ya baharini.

WAZIRI wa Uchumi wa Bluu na Maendeleo ya Uvuvi ,Abdallah Ali Kombo (wa pili kulia) akikata utepe kuzindua mpango wa kuwasaidia wavuvi unaotekelezwa na Kampuni ya Salmin Fisheries unaofadhiliwa na benki ya Equity ikiwa ni sehemu ya mbinu za utekelezaji wa dhana ya uchumi wa bluu. (PICHA NA MPIGA PICHA WETU).

 


Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango