Wizara yajipanga kuongeza ufanisi
awamu ya pili TASAF
NA MWANDISHI WETU
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar
imesema itahakikisha utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi wa kunusuru kaya
maskini unaofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) unaangalia
mahitaji ya walengwa na wanaostahiki kupatiwa huduma zikiwemo za fedha taslimu.
Hatua hiyo imeelezwa itawezekana kwa
kuwashirikisha wakaazi wa vijijini na shehia husika ili kupatikana kwa walengwa
wanaokusudiwa kuingia katika mpamgo huo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,
Sera, Utatibu na Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid Salum Mohamed, alieleza hayo
wakati akizungumza na wajumbe wa Kamati ya kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa
Serikali katika ukumbi wa wizara hiyo Vuga, mjini Zanzibar.
Alisema utekelezaji huo unalenga
kuimarisha maisha ya kaya maskini kupitia mradi huo yanatimia na watendaji
wanaosimamia jukumu hilo wanatimiza
masharti na vigezo vilivyowekwa katika kuzifikia kaya hizo.
Alisema, eneo jengine ambalo litakalosimamiwa
ipasavyo ni kuona miradi inayoekezwa ndani ya jamii iwe yenye mahitaji ya watu
wa maeneo husika na kuleta manufaa ndani ya jamii.
Alisema, miradi inayofadhiliwa Mfuko
wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) inalazimika kuzingatia sheria na kufuatia
miongozo iliyowekwa na serikali badala ya maslahi binafsi ya viongozi wa
majimbo au watendaji wa serikali.
“Lazima viongozi na watendaji
wanaosimamia miradi ilyopo chini ya TASAF wafuate sheria na taratibu zilizopo
bila ya kujali ama kuangalia maslahi binafsi ya viongozi,” alieleza waziri
huyo.
Akizungumzia fedha za mfuko wa
jimbo, Dk. Khalid, alisema ofisi yake haitokuwa na muhali badala yake
itahakikisha inasimamia sheria na taratibu zilizowekwa kuhakikisha fedha hizo
zinaleta tija kwa umma.
“Nitakuwa mkali na kufuatilia kwa
karibu matumizi ya fedha za mfuko wa jimbo kwani zinatolewa kwa ajili ya
kuimarisha huduma za jamii hivyo viongozi lazima tuheshimu sheria zilizopo,” alisema.
Nae Mratibu wa TASAF Ofisi ya
Makamu wa Pili, Khalid Hamrani, alisema wa awamu ya pili ya mradi huo, utawashirikisha
ipasavyo watendaji wa ofisi hiyo na ambae
atabainika kwenda kinyume ma utaratibu atachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.
Alisema hatua hiyo imekuja baada ya
kubaini kuwepo kwa changamoto zilizojitokeza katika mradi uliomalizika kwa
kuorodheshwa watu wengine ambao waliokuwa sio walengwa.
“Waajiriwa wa serikali katika ofisi
yetu ndio tutakaowatumia na asiewajibika vyema sheria itachukua mkondo wake
ikiwa ni pamoja na kukatwa mshahara pale itapobainika ametoa fedha kwa mtu
ambae sio mlengwa,” alisema.
Alifahamisha kuwa mradi huo ambao
unatarajiwa kuanza kutekelezwa Febuari mwaka huu tayari uhakiki umeshafanywa na
hata hivyo zoezi la kushirikishwa jamii katika utambuzi wa walengwa
litasimamiwa ipasavyo.
Alifahamisha miongoni mwa mambo
mengine yatakayotekelezwa katika mradi huo awamu hii ni kutumia teknolojia kuwatambua
ili kuthibiti watu wasio walengwa.
Alisema utafiti uliofanywa umebaini
Zanzibar kulikuwa hakuna wanufaika hewa ndani ya mradi huo isipokuwa kulikuwa
na idadi kubwa ya walengwa wasiostahiki hali iliyochangiwa na wasimamizi wa
walengwa wa mradi huo (SMC).
Alisema watu wengine waliobainika
katika utafiti huo ni kuandikishwa watu wasio na sifa ya kuingia katika mradi
huo.
Mapema Mwakilishi wa jimbo la
Ziwani, Suleiman Makame Ali, alimuomba Dk. Khalid kusimamia kwa karibu mradi
huo hasa ikizingatiwa wapo baadhi ya masheha wamekuwa wakitumia fursa hiyo kwa
kuingiza familia au watu wakatibu na wale walengwa wakaendelea kukosa kuitumia
fursa hiyo.
Comments
Post a Comment