DC Suzan ataka waliokopa warudishe mikopo kwa wakati
NA MWANDISHI WETU
MKUU
wa Wilaya ya Magharibi ‘A’, Suzan Peter Kunambi (pichani), amewataka wanaushirika wa kuweka
na kukopa Kibweni (Kibweni Saccos) kurejesha mikopo kwa wakati ili kuendeleza
ushirika huo.
Alisema
hayo katika Skuli ya Bububu, wilayani humo alipofungua mkutano mkuu wa mwaka wa
chama hicho na kusema umefika wakati kwa wanaushirika kutilia mkazo umuhimu wa
kurejesha mikopo katika vyama vyao na faida inayopatikana iwanufaishe wote.
Alisema
tabia ya wanachama kuchukua mikopo kisha kushindwa kurejesha kwa wakati inasababisha
vyama vya ushirika kushindwa kujiendesha wenyewe na na hatimae kusubiri
wahisani.
Kunambi
alisema vyama vya ushirika ni muhimu katika maendeleo ya nchi na inasaidia
kuinua uchumi kwa mwananchi mmoja mmoja hivyo aliwataka wanaushirika kuibua
miradi ya maendeleo kuendeleza vyama hivyo.
Aidha
aliwapongeza wana ushirika hao kwa kuanzisha ushirika imara ambao umekuwa mfano
ndani ya wilaya hiyo na kuwahamasishana wananchi wengine kuingia katika
ushirika huo ili kuongeza idadi ya wananchama na kuleta mabadiliko ya
kiutendaji.
“Tunahaki
ya kuwaelimisha na wengine waingie kwenye ushirika huu tupate maendeleo ya
kweli kupitia vyama vya ushirika,” alisema.
Akizungumzia
suala la udhalilishaji wa kijinsia, aliwataka wanaushirika hao kupiga vita
vitendo hivyo katika jamii ili kuwanusuru watoto na wanawake dhidi ya vitendo
hivyo.
Mapema
Mrajis wa vyama vya ushirika Wilaya ya Magharibi ‘A’, Abulmajid Masoud Khalfan,
alisema licha ya mafanikio yaliyopatikana kwa wanaushirika huo lakini elimu juu
ya masuala ya mikopo inahitajika kwa wanachama wake pamoja na mbinu za
kuendesha biashara ndogondogo na kubwa kwenye ushirika wao.
Nae
Mwenyekiti wa ushirika huo, Abdurahman Khalfan, alisema wanakabiliwa na ukosefu
wa kiwanja pamoja na jengo la kuendeshea ushirika wao hali inayosababisha
kuendeleza harakati zao kwenye jengo la kukodi.
Hata
hivyo walimuomba Mkuu huyo kuwapatia eneo ili wajenge ofisi ya kudumu na badala
yake waondokane na usumbufu wanaoupata kwa kuazima jengo.
Akisoma
risala Mjumbe wa kamati ya uongozi wa ushirika huo, Mboja Muhidini Masoud,
alisema ushirika huo umepiga hatua kwa kukopeshawa mikopo kutoka shilingi
50,000 hadi kufikia shilingi 8,000,000 kwa mtu mmoja mmoja.
SACOS hiyo ilianzishwa mwaka 2007 na kupata usajili mwaka 2008 ilianza na wanachama 66 wanawake 55 na wanaume 11 na hadi sasa ina wanachama 108.
Comments
Post a Comment