Skuli ya Upendo yapongezwa kutoa mwanafuzi
bora kitaifa
Yatoa wanafunzi watatu bora kitaifa mitihani STD 4, Veronica Mwendesha ashika nafasi ya kwanza Zanzibar
NA MWINYIMVUA NZUKWIVIONGOZI wa jimbo la Bububu, wilaya
ya Magharibi ‘A’, Unguja, wameeleza kuwa wataendelea kutoa kipaumbele kwa
maendeleo ya jamii ikiwemo elimu ili kupata taifa linalojitegemea kwa wataalamu.
Kauli hiyo imetolewa na Diwani wa wadi ya Dole, Juma Wiliam Sungwa, kwa niaba ya Mwakilishi wa jimbo hilo Mudrik Ramadhan Soraga, katika hafla ya kuwapongeza wanafunzi wa skuli ya maandalizi na msingi, Upendo iliyopo shehia ya Kizimbani Unguja, iliyotoa mwanafunzi bora kitaifa katika mitihani ya darasa la nne iliyofanyika mwaka uliopita Zanzibar.
Alisema mafaniko ya skuli hiyo
kutoa wanafunzi watatu katika nafasi tano za juu kitaifa katika mitihani hiyo
ni ya kupongezwa na inapaswa kuungwa mkono na kila mmoja miongoni mwa wananchi
wa jimbo hilo.
Alifafanua kuwa licha ya kuwa
skuli hiyo kumilikiwa na taasisi binafsi, bado serikali na viongozi hao
wanapaswa kuisadia kutokana na mchango inaoutoa katika ujenzi wa taifa la
wasomi watakaoitumikia Zanzibar.
“Kutoa wanafunzi watatu katika
nafasi tano za juu kitaifa sio mafanikio ya kupuuzwa, lazima tujivunie kuwa na
mwanafunzi bora kitaifa lakini kujipanga kuhakikisha watoto wetu wanafikia
malengo yao,” alisema Sungwa.
Akizungumzia changamoto
zinazoikabili skuli hiyo na nyengine ndani ya jimbo hilo, Sungwa alisema
zitapatiwa ufumbuzi hatua kwa hatua kwa kushirikiana na manispaa ya Magharibi
‘A’, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na wadau wengine wa elimu wa
ndani na nje ya jimbo hilo.
“Hili la upungufu wa vitabu vya
kiada na ziada vinavyofuata mtaala wa SMZ, tunalichukua pamoja na zile
changamoto nyengine na katika muda mfupi ujao tutalipatia ufumbuzi,” alisema
diwani huyo.
Akizungumza katika hafla hiyo
iliyoambatana na utoaji wa zawadi kwa wanafunzi waliofanya vyema na wengine wa
skuli hiyo, mdhamini wa skuli hiyo, Younggum Park (Mama Park), alipongeza
juhudi za wazazi na walezi wa skuli hiyo kwa kutoa kipaumbele cha elimu kwa
watoto wao.
“Katika baadhi ya maeneo, watu
hawaipi elimu kipaumbele cha kwanza kwa watoto wao hasa wasichana, lakini watu
wa eneo hili wamekuwa tofauti, ninawapongeza sana,” alieleza Mama Park.
Akisoma risala ya skuli hiyo,
mwalimu Ezekiel Jackson, alieleza kuwa mwaka 2020, skuli hiyo iliyoanzishwa mwaka
2016, imetoa wanafunzi watatu katika nafasi ya kwanza, nafasi ya tatu na ya nne
katika mitihani ya darasa la nne kitaifa.
“Kwetu haya ni muendelezo wa
mafanikio, kwani katika mwaka 2019 tulifanikiwa kutoa mwanafunzi alieshika
nafasi ya kwanza kitaifa katika mitihani ya darasa la nne kiwilaya, kimkoa na
kitaifa kama ilivyokuwa katika mwaka 2020,” alieleza mwalimu huyo.
Ezekiel aliwataja wanafunzi
waliopata ufaulu huo kuwa ni Veronica Paulo Mwendesha alieshika nafasi ya
kwanza, Christina Kurwa alieshika nafasi ya tatu na Sleyum Rashid Said,
alieshika nafasi ya nne ambap skuli hiyo ilifaulisha wanafunzi 22 kwa daraja
‘A’, wawili daraja ‘B’ na mmoja daraja ‘C’.
Hivi karibuni akizungumza katika
hafla ya kuwapongeza wanafunzi waliofaulu michepuo katika skuli ya Langoni
Msingi, Mkurugenzi Msaidizi Elimu, manispaa ya Magharibi ‘A’, mwalim Ahmed
Abdulmajid aliyataja matokeo hayo kuwa ni mafanikio ya kujivunia na yanayohitaji
kuendelezwa.
“Katika mitihani iliyopita,
wilaya yetu ilishika nafasi ya kwanza katika mitihani ya darasa la nne na zaidi
ya wanafunzi watatu walitokea katika nafasi 10 bora katika kiwilaya na kimkoa,
haya ni mafanikio makubwa hasa kwa watoto wa maeneo haya,” alieleza.
Akielezea mikakati ya baadae, Mwalimu
Mkuu wa skuli hiyo Elia John Maleso, alisema ni kuendelea kufanya vyema hivyo
aliwaomba wananchi kuendelea kushirikiana na kuwapongeza viongozi hao wa jimbo
kwa kutambua mafanikio ya skuli hiyo.
“Lengo letu ni kushika nafasi ya
kwanza kila mwaka na kwa kuzingatia kuwa mwaka huu tutakua na darasa la sita,
niwaombe wazazi waendelee kuwasaidia watoto wao kufaulu michipuo na kujenga
msingi bora wa maisha yao,” alieleza mwalimu Elia.
Katika mahafali hayo mbali ya
zawadi ya vifaa vya skuli, mwanafunzi Veronica Paulo Mwendesha na wenzake
walikabidhiwa zawadi mbali mbali zilizotolewa na madiwani wa jimbo la Bububu na
Mama Park anaeidhamini skuli hiyo.
PICHA.
Comments
Post a Comment