SMZ yaahidi mazingira mazuri kuibua viongozi wanawake

NA MWANDISHI MAALUM

IMEELEZWA kuwa iwapo kutawekwa mazingira mazuri ya sera na sheria kuna uwezekano mkubwa wa kuongeza idadi ya viongozi wanawake serikalini na katika vyombo vya maamuzi.

Akizindua muongozo wa ‘ushiriki wa wanawake katika uongozi’, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena Ahmed Said, alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) itafanya hivyo kuunga mkono juhudi asasi za kiraia zilizolenga kutoa kipaumbele kwa mwanamke katika nafasi za uongozi.

Uzinduzi wa muongozo huo ulioandaliwa kwa pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Chama cha Wanasheria Wanawake (ZAFELA) na Jumuia ya Jinsia na Utetezi wa Mazingira Pemba (PEGAO), ulifanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul Wakil,  Kikwajuni mjini Unguja Februari 14, 2021.

Mhandisi Zena, alisema serikali ya awamu ya nane itajitahidi kuondoa vikwazo vyote, ikiwemo urasimu ili kuhakikisha wanawake wanapewa fursa na nafasi za uongozi bila kwa kuzingatia uwezo wao.

“Tunahitaji kuwa na Zanzibar yenye uwiyano wa kijinsia katika uongozi, hivyo suala la jinsi lisiwe kikwazo cha kutompa fursa mwanamke kuwa kiongozi kwani mwanamke akipewa nafasi anaweza na anawajabika ipasavyo kuiletea maendeleo jamii yake,” alisema Mhandisi Zena.

Aidha alizipongeza asasi za kiraia kwa jitihada zao za kuandaa miradi ya kuwahamasisha wanawakae kujiinua kwenye masuala ya uongozi na mambo mengine yakiwemo ya kiuchumi.

Alisema kupitia mradi huo waliouzindua, utasaidia kuleta hamasa na shauku kubwa kwa wanawake wa Unguja na Pemba katika kushiriki kwenye masuala ya uongozi, kwani mwanamke anapopewa fursa anaweza.

Alieleza kuwa serikali inatambua kuwa jinsi ya kike inakumbana na changamoto mbali mbali ikiwemo ya kasumba ya mfumo dume uliojengeka katika jamii kuwa mwanamke ni mtu wa kuongozwa. 

Alikitaja kikwazo kingine kuwa ni kutokuwepo na utayari wa wanawake wenyewe kushiriki kwenye mambo mbali mbali ya kijamii jambo linalopaswa kupigwa vita.

“Natamani jamii kuamka na kujua na umuhimu wa mwanamke katika suala zima la uongozi, kwani ikiwa yeye ndie mlezi wa kwanza katika familia, basi pia ni mtu imara katika masuala ya uongozi.

Akizungumzia mradi huo wa ushiriki wa wanawake katika uongozi, Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jamila Mahmoud, alisema mradi huo wa miaka minne umelenga kuwajengea uwezo wanawake ili wawanie nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao.

“Lengo la mradi huu ni kuwahamasisha na kuwajengea uwezo wanawake ili kuingia katika michakato ya kutafuta uongozi,” alisema Jamila.

Kwa upande Mkurugenzi wa Chama cha wanahabari wanawake (TAMWA) ofisi ya Zanzibar, Dk. Mzuri Issa Ali, alieleza kuwa kwa kipindi kirefu wanawake walikua nyuma katika masuala ya uongozi lakini baada ya jitihada na kuhamasishwa walianza kujitokeza ingawa bado ushiriki wao katika vyombo vya maamuzi bado mdogo. 

“Katika ngazi za juu za kisiasa hususani kwenye suala la maamuzi huwaoni wanawake, imekua kama tumeekewa kikomo cha kuongoza” alisema Dk. Mzuri.

Alisisitiza kuwa, ili kufikia huko Lazima kuwe na jitihada za pamoja katika kumpa nguvu mwanamke kwani wanawake wana mchango mkubwa katika kuongoza na masuala mazima ya demokrasia.

“Kupitia muongozo huu, matumani yetu utatoa fursa kwa wanawake ya kujipanga kwa miaka ya mbele na kuona ni namna gani wanaweza kujitokeza katika masuala ya uongozi,” alisema Mzuri.

Katika uzinduzi huo, viongozi mbali mbali wa serikali, vyama vya siasa na kijamii wanawake na wanaume walishiriki huku wakizipongeza asasi hizo kwa hatua waliyofikia ambayo waliitaja kuwa itaongeza ushiriki wa wanawake katika kuwania nafasi za uongozi.

 

 

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango