Wizara ya utalii, mambo ya kale yatoa muongozo kulinda maadili
NA KHADIJA KHAMIS, MAELEZO - ZANZIBAR
WAZIRI
wa Utalii na Mambo ya Kale, Lela Muhamed
Mussa, ametoa muongozo kwa wageni na watalii wanaoingia
nchini kufuata maadili yanayohusiana na mavazi ili kwenda sambamba
na mila silka maadili na utamaduni wa kizanzibari .
Akitoa
taarifa kwa vyombo vya habari alisema hivi karibuni kumejitokeza ukiukwaji
wa maadili hususani katika suala la mavazi kwa baadhi ya wageni na watalii
wanaotembelea nchini.
Alifahamisha
kuwa wageni na watalii wanatakiwa kufuata maadili ya nchi kwa kuvaa nguo za
stara wanapokuwa katika sehemu za umma ili
kuepusha kero na maudhi kwa wananchi.
Alieleza kuwa
kushindwa kuifuatilia na kuisoma miongozo ya maadili ambayo imekuwa ikitolewa
na taasisi zinazosimamia utalii nchini ni miongoni mwa sababu zinazopelekea
utaratibu mbaya wa mavazi kwa wageni hao.
Waziri Lela,
alisema hali hii haitoi sura nzuri na inaashiria kutokuwepo uwajibikaji wa
pamoja na mashirikiano kwa baadhi ya wananchi au taasisi ambazo zinashindwa
kusimamia suala la maadili kwa wageni na watalii wanaoingia nchini.
Alisema
serikali haipendezeshwi na hali ya kivazi kwa wageni na watalii ikiamini kwamba
pamoja na kuhitaji utalii kwa maslahi ya wananchi na serikali kwa ujumla lakini
inaheshimu suala la maadili ya jamii.
Alieleza
kuwa kutokana na kutoridhishwa na hali hiyo, Wizara ya Utalii na
Mambo ya Kale imeona haja ya kusisitiza umuhimu wa kusimamia maadili kwa
watalii kwa vile mila, silka na utamaduni wa Zanzibar ambao ni urithi na
ni miongoni mwa vivutio vya utalii .
Waziri
huyo alizitaka jumuiya zenye kuandaa misafara ya kitalii nchini, kutambua zimabeba jukumu la kuleta wageni kuzingatia
kanuni za mwaka 2015 kifungu cha 51 (b) inayozipa jukumu la kuhakikisha watalii
wanaowasimamia wanafuata sheria pamoja na kuwapatia kanuni za maadili kwa
watalii kabla ya kuwafikisha nchini pamoja na kuwasimamia kufuata maadili hayo
wanapoingia nchini.
Hata
hiyo alisema kwa upande wa wenye Mahoteli na mikahawa ya kitalii
kuwa na wajibu wa kutoa taarifa kuhusiana na miongozo ya maadili kwa
watalii na wageni na ni marufuku kwa wenye kuendesha biashara ya hoteli
kuwavisha nguo zisizo na stara wafanyakazi wao .
Wizara
inaviomba vyombo vya ulinzi na usalama nchini kushirikiana pamoja na wadau
wengine wa utalii katika kukabiliana na kadhia hiyo.
Alifahamisha
Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale imeshawasiliana na ofisi za kibalozi za Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania katika nchi mbali mbali duniani na kuwapatia
maadili ya utalii wa Zanzibar.
Comments
Post a Comment