Ayoub ataja vipaumbele Kaskazini Unguja, apiga marufuku ‘vigodoro’
MWASHUNGI TAHIR, MAELEZO
MKUU
wa Mkoa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud, ameeleza kuwa serikali
ya huo umelenga kukuza sekta ya utalii kwa kuvitangaza na kuviendeleza vivutio
vya utalii vilivyomo mkoani humo.
Ayoub
alieleza hayo ofisini kwake Mkokotoni, alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari kuzungumzia utekelezaji wa kazi za serikali ya mkoa huo katika kipindi
cha miaka mitano ijayo.
Alieleza
kuwa mkoa huo una vivutio vingi na maeneo ya mahoteli na mikahawa mikubwa,
fukwe zinazovutia na maeneo ya kihistoria ambayo wageni na wenyeji wanapasa
kuyajua.
Aliongeza
kuwa pamoja na kuimarisha sekta hiyo, katika kipindi cha miaka mitano pia mkazo
zaidi utawekwa katika ukuzaji wa sekta zinazokuza ustawi wa jamii zikiwemo za kilimo,
mifugo, maji safi na salama, elimu, afya, miundombinu ya barabara na michezo.
“Pia
kwa kuzingatia mipango ya serikali kuu, serikali ya mkoa itaendelea kuhamasisha
ujenzi wa viwanda vipya na kuviendeleza vilivyopo ili kukuza ajira lakini pia
wakulima wetu wapate soko la mazao wanayozalisha,” alieleza Ayoub.
Alisema
hatua hiyo itaimarisha uzalishaji wa mazao mbali mbali yakiwemo ya mananasi na
mboga mboga ili wakulima wapate kuepukane na hasara katika mazao yao wanayolima
kila msimu.
Sambamba
na hayo alisema serikali ya mkoa kwa kushirikiana na serikali kuu, imejipanga kudhibiti
vitendo vya udhalilishaji, matumizi ya dawa za kulevya na rushwa kwa kutovifumbia
macho kwani vinarudisha nyuma maendeleo ya taifa.
Aidha
Ayoub aliahidi kulisimamia suala la kilimo cha umwagiliaji maji, kuimarisha ufugaji
na kuweka mazingira kuwa katika hali ya usafi.
Sambamba
na hayo, katika kuimarisha maadili, amepiga marufuku ya upigaji ngoma za
vigodoro pamoja na khanga moja katika maeneo ya mkoa huo kwa kuwa zinaenda
kinyume na mila, silka na utamaduni wa Zanzibar.
“Kuanzia leo si ruhusa kwa wakaazi wa mkoa huu
na wananchi kutoka sehemu nyengine kuja kupiga ngoma na kucheza ngoma
hizo kwani zimekosa maadili”, alisema Ayoub.
Katika
taarifa yake hiyo ayoub pia alipongeza juhudi za rais wa Zanzibar na mwenyekiti
wa baraza la mapinduzi, dk. Hussein ali mwinyi na kuahidi kutekeleza maagizo
yote aliyoyatoa ili kuongeza ufanisi.
Hivyo
aliwataka watendaji wa mkoa huo kuacha kufanya kazi kwa mazowea badala yake
kujidhatiti kufanya kazi kwa bidii, maarifa na weledi ili kuongeza tija katika
utoaji wa huduma kwa wananchi.
Comments
Post a Comment