Dk. Mwinyi ahimiza mageuzi sekta ya kilimo
NA RAJAB MKASABA, IKULU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameitaka wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kuiimarisha sekta ya kilimo kwa kukifanya kuwa cha biashara na kilete tija.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo jana ikulu jijini Zanzibar, alipokutana na uongozi na watendaji wa wizara kwa ajili ya kutoa taarifa ya utekelezaji wa maagizo kwa mawaziri na Makatibu Wakuu wa wizara za SMZ wakati alipowaapisha.
Alieleza kuwa ipo haja kwa Wizara hiyo kuangalia uwezekano wa kilimo kuwa cha biashara na cha kisasa hatua ambayo itawasaidia hata wakulima kunufaika zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.
Alisema kuwa kilimo kinachofanyika hivi sasa hakijawa na faida kwa wakulima na hata serikalini kwani lile lengo lililokusudiwa la kuhakikisha chakula cha kutosha hasa mchele unazalishwa hapa Zanzibar halijafikiwa.
Aidha, kwa upande wa ufugaji, Dk. Mwinyi alisema kuna tatizo kwa sababu wafugaji hawajaweza kusaidia hivyo, ni vyema kukatafutwa wafugaji wakubwa waweze kuendesha shughuli hizo na hatimae wapate kuwasaidia wafugaji wadogo.
Alieleza azma yake ya kutaka mabadiliko katika sekta ya kilimo na sekta hiyo iondoke hapa ilipo na iweze kuwa na tija na mafanikio makubwa.
Alisisitiza umuhimu wa kuweka utaratibu maalum wa kutafuta wawekezaji wa kilimo kwa kupitia Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) huku akisisitiza haja ya kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wa ufugaji.
Alieleza matarajio yake kuona kwamba sekta ya kilimo inaimarika zaidi kutokana na bajeti ya kutosha kinyume na kile kinachopatikana katika sekta hiyo.
Dk. Mwinyi, alikemea tabia ya kufanya kazi kwa mazoea na kusisitiza haja kwa wizara hiyo kufanya kazi zake kwa lengo la kupata tija kwa kuimarisha kilimo ambacho kitazalisha chakula cha kutosha hapa Zanzibar badala ya kuagizia nje ya nchi.
Alieleza haja kwa Wizara hiyo kuliangalia suala upatikanaji wa pembejeo na faida yake huku akieleza kwamba shughuli za karakana na huduma za matreka zifanywe kibiashara hali itakayopelekea kujiendesha.
Akieleza suala zima la ugawaji wa mashamba kwa wananchi wa kisiwani Pemba, alieleza haja ya kuwepo kwa utaratibu mzuri wa ugawaji wa mashamba hayo ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wakuu wa mikoa na wilaya ili kuepuka migogoro.
Awali Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Mariam Juma Abdalla alieleza kuwa wizara ina lengo la kufanya mageuzi katika sekta ya kilimo kuwa cha kisasa, jumuishi na chenye ushindani ambacho kitachangia sekta ya viwanda na utalii.
Aidha, alisema kuwa sekta ya kilimo inatoa ajira rasmi kwa wastani wa asilimia 40 na zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wanategemea sekta hiyo kwa njia moja au nyengine katika kujipatia kipato na kuimarisha maisha yao.
Alisema kuwa wizara hiyo imechukua hatua mbali mbali za kuanzisha mahusiano kwa kuwapatia wakulima na wafugaji mikopo nafuu kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB), Benki ya PBZ na CRDB.
Aidha, katibu huyo alieleza kwamba wizara imejiunga na mtandao wa kielektroniki (SNR Mwinyi) kwa ajili ya kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi changamoto za wananchi.
Alisema kwamba wizara hiyo, inaendelea kupambana na wadudu waharibifu wa matunda kwa kusambaza mitego ya kunasa wadudu hao na kutoa taaluma kwa wakulima katika kukabiliana na wadudu waharibifu na maradhi ya kupitia halmashauri
Alisema wizara inashauri serikali iyatoe
mashamba ya eka tatu 6,315 ambayo tayari yameshatambuliwa kisiwani Pemba kwa
wananchi wenye nia ya kuyaendeleza.
video:
Comments
Post a Comment