Dk. Mwinyi awataka wananchi kuwa watulivu kifo cha JPM

NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewataka Watanzania kuwa watulivu kufuatia kifo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, Dk. Mwinyi pia alituma salamu za rambirambi kuwataka kuwa na moyo wa subira Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Mjane wa marehemu Mama Janeth Magufuli, familia yake na wananchi Tanzania.

Alisema kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Wananchi wote wa Zanzibar anatoa salamu hizo na kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.

“Huu ni msiba mzito sana kwangu na kwa taifa letu la Tanzania, hivyo nakuombeni tuwe na subira na tuwe watulivu,” alieleza Dk. Mwinyi katika taarifa yake.

Dk. Magufuli alifariki jioni ya Machi, 17 mwaka huu kwa maradhi ya moyo katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu taarifa ambayo ilitolewa na mama Samia usiku wa kuamkia jana.

Katika taarifa yake, samia alieleza kuwa Dk. Magufuli awali alipatiwa matibabu katika hospitali ya moyo ya Jakaya Kikwete ambapo alilazwa kwa siku kadhaa na kuruhusiwa kabla ya kurudishwa hospitalini hadi mauti yalipomkuta.

Machi 19, Dk. Mwinyi alikuwa miongoni mwa viongozi wa kitaifa kutia saini kitabu hicho cha maombolezi  katika viwanja vya ukumbi wa Karimjee, ulioko Jijini Dar es Salaam na kueleza jinsi alivyopokea kwa mshtuko mkubwa kifo cha kiongozi huyo.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza jinsi Hayati Rais Magufuli alivyoitumia nchi kwa nidhamu kubwa sana ikiwa ni pamoja na kusimamia  kiuchumi na kimaendeleo kwa misingi ya amani, utulivu, umoja na mshikamao.

Vile vile Dk. Mwinyi aliungana na waumini wa dini ya Kislamu katika sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Masjid Maamur Upanga, Jijini Dar es salam kabla ya kwenda kumfariji na kumpa pole Mjane wa Hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huko Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Dk. Mwinyi akiwa na mkewe Mama Mariam Mwinyi walimpa pole Mjane wa Marehemu Hayati Magufuli Mama Janet Magufuli na kumtaka awe na subira yeye pamoja na familia yake katika kipindi hichi kigumu cha msiba.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alishiriki kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan mara tu baada ya kuapishwa na kushika wadhifa huo wa Urais. 

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango