Dk. Mkuya ahimiza uwajibikaji taasisi zilizo wizarani kwake

RAYA HAMAD, OMKR

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Dk. Saada Mkuya Salum,  amewataka watendaji na wafanyakazi wa Tume ya Kuratibu na Udhubiti wa Dawa za Kulevya, kuongeza juhudi zamapambano dhidi ya wanaoingiza, kuuza na kusambaza kwa maslahi ya Zanzibar

Dk. Saada ameeleza hayo alipokutana na uongozi na wafanyakazi wa tume hiyo na kuwasisitiza kuwa waadilifu na waaminifu kwa vile ya matumizi ya dawa za kulevya ni kero katika jamii na mtandao wake ni mkubwa

Ameeleza kuwa katika kusimamia vyema utekelezaji wa majukumu ya tume hiyo Dk.  Saada, amewataka kuzidisha mashirikiano na taasisi mbalimbali wanazofanya kazi kwa ukaribu ikiwemo Uwanja wa ndege, Bandarini,  kikanda, kitaifa na kimataifa na kusambaratisha mitandao wa wahalifu

Pia amewakumbusha kuwa hivi sasa fursa nyingi za maendeleo zinapatikana zikiwemo utalii ujenzi wa miundo mbinu ambazo zimekuwa zikiibua fursa mbali mbali za kiuchumi  na kuiwa na maingiliano jambo ambalo wahalifu wa madawa ya kulevya nao hugeuza fursa kwa upande wao na kutumia mwanya huo kuingiza madawa ya kulevya

Aidha waziri huyo  amewahimiza watendaji kuvitumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kufikisha elimu kwa wananchi pamoja na kufanya tathmini juu ya kile wanachokitoa hatua ambayo itasaidia kufahamu mapungufu yaliyopo kwa upande wao

Amesema atahakikisha anashirikiana na watendaji na  anasimamia vyema sheria na sera  ikiwemo kuzipitia upya na kufanya marekebisho pale panapohitajika kufanya hivyo ili kuwabana wahalifu na kuifanya jamii na Serikali  iwe huru

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo, Kheriyangu  Mgeni Khamis,  amesema pamoja na mambo mengine tume imefanikiwa kuteketeza dawa za kulevya kitaalamu , kuanzishwa kwa nyumba za kurekebisha tabia, kufanya marekebisho ya Sheria 2019 na kubadilisha vifungu vya adhabu, kuimarisha mashirikiano ya  kitaifa na kimataifa

Ameeleza kuwa kupungua kwa  unyanyapaa kwa wanaochana na matumizi ya dawa za kulevya, kubadilika na kukubalika kwa familia zao ambao awali waliwakataa kutokan na tabia ya matumizi ya dawa za kulevya

Wakati huo huo Dk. Saada, ametembelea ofisi za Tume ya Ukimwi Zanzibar (ZAC) na kuwaomba watendaji wa tume hiyo kuharakisha utoaji wa muongozo na kufanyiwa kazi, ikizingatiwa kuwa watendaji wakuu wengi ni wapya ili wapate fursa ya kuupitia

Amesema pamoja na kuwa ZAC kujitihidi kutoa elimu, bado kuna haja ya kutilia mkazo kwa baadhi ya maeneo korofi, taasisi za wafanyakazi sehemu za utalii na kwengineko ili kuepusha maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi pamoja na kuwaandalia mazingira bora ya watu wanaoishi na virusi hivyo.

Amewataka watendaji wasiridhike na kiwango cha maambukizi cha sasa cha asilimia 0.4 kwa vile maaingiliano ni makubwa hasa kwa wakati huu ambao Zanzibar inapata wageni wengi aidha matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii nayo inachochea masuala ya kujamiiana hasa kwa vijana

Nae Mkurugenzo Mtendaji wa Tume ya Ukimwi, Dk. Ahmeid Mohammed Khatib Reja, amesema moja kati ya mafanikio ya tume ni jamii imeelimika na hivyo kupunguwa kwa unyanyapaa, tokea ukimwi ulipoingia Zanzibar haijawahi kuvuka kiwango cha asilimia 1 ukilinganisha na mataifa mengine ambapo kiwango huwa juu.

Hata hivyo ameelezea changamoto na matarajio tume hio ambapo amesema kuongezeka kwa tabia hatarishi na matendo maovu ya udhalilishaji kama ubakaji na kujamiiana kusiko salama bado ni changamoto

Aidha alieleza kuwa tume imejipanga kuzijengea uwezo baadhi ya Shehia zilizoko ukanda wa pwani ambako utafiti wao wameona haziko salama kutokana na maingiliano na watu wenye mazingira na tabia tofauti ili vijana na wazee waweze kufahamu mazingira hatarishi na namna ya kukabiliana nazo.

 

 

 

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango