Siku ya uhuru wa habari kuadhimishwa kimkakati Zanzibar
NA ASYA HASSAN
UMOJA wa Taasisi za Waandishi wa Habari
Zanzibar, kupitia kamati maalum, unatarajia kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo
vya habari kwa kutoa tunzo kwa waandishi watakaoandika habari zitakazotoa
matokeo chanya kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Farouk
Karim, alieleza hayo jana katika mkutano na waandishi wa habari, katika ukumbi
wa Idara ya Mawasiliano na Taaluma za Habari ya chuo kikuu cha Zanzibar (SUZA),
Kilimani wilaya ya Mjini Unguja.
Alisema hatua hiyo itasaidia waandishi
kuongezea ujuzi, kujiamini, kujituma na kuongeza ubora katika kazi zao.
Alifahamisha kwamba tunzo hizo
ambazo zimeegemea katika maeneo makuu matano ambayo ni uandishi wa habari za uchumi
wa buluu iliyopewa jina la ‘Dk. Hussein Mwinyi Award’, Uandishi wa Habari za
Jinsia (Mama Mariam Mwinyi Award), Uandishi wa Habari za Serikali ya Umoja wa
Kitaifa (Maalim Seif Award), Uandishi wa Habari za Rushwa na uwajibikaji (ZAECA
Award) na Uandishi wa Habari za kulipa kodi (ZRB Award).
Alivitaja vigezo vitakavyotumika
kupata tunzo hizo ni pamoja na ubora wa kazi iliyowasilishwa, upekee wa
mada, umuhimu wa kuzingatia uwiano usawa wa kijinsia, ubunifu wa mada husika na
matokeo baada ya kutoka habari au kipindi hicho.
Mwenyekiti huyo alisema ni vyema
waandishi hao kujituma na kuchangamkia fursa hiyo kwani itawasaidia katika utekelezaji
wa majukumu yao ya kila siku sambamba na fursa ya waandishi wa habari wa
Zanzibar kuonesha uwezo wao, weledi na umahiri katika kazi zao.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dk.
Mzuri Issa Ali, alisema wameamua kuweka tunzo hizo ili kuisaidia kukuza vipaji vya
waandishi wa habari na kwamba hatua hiyo inalenga kukuza maslahi makubwa kwa
nchi kutokana na kazi hizo kuonesha vitu mbali mbali ambavyo vikifanyiwa kazi
vitaleta matokeo chanya kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
“Kazi hiyo sio rahisi kwani tumejipanga
na kuna majaji imara ili mtu aweze kushinda itapitiwa na kuangaliwa vitu
mbalimbali, hivyo mtu akishinda atakuwa amefanya kazi na anahitaji kupata tunzo
hiyo,” alisema.
Kwa upande wake Katibu wa kamati hiyo
Salma Said, alisema malengo ya maadhimisho hayo ni kuongeza hadhi ya uandishi
wa habari na thamani ya waandishi wa habari ikiwa ni pamoja na kuandika habari
kwa ufanisi, kufatilia, kutafuta na zenye kiwango cha juu.
“Uamuzi huu unatokana na sisi kama
viongozi wa taaisisi kukubaliana kuwa habari nyingi zinazoandikwa hazina
viwango vizuri kiasi cha kuleta matokei makubwa,” aliongeza Salma.
Siku ya uhuru wa vyombo vya habari kimataifa
huadhimishwa Mei 3 ya kila mwaka, lakini kutokana na siku hiyo kuangukia katika
mwezi mtukufu wa Ramadhani, taasisi za Zanzibar zitaiadhimisha siku hiyo Mei 23,
mwaka huu.
BAADHI ya wawakilishi wa taasisi za kihabari zinazoandaa maadhimisho ya siku ya uhuru wa habari duniani wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa mkutano wa waandishi wa habari jana. kutoka kushoto mstari wa mbele ni Salma Said (WAHAMAZA), Farouk Karim (ITV/RADIO 1), Dk. Mzuri Issa (TAMWA - Z'BAR) . Mstari wa nyuma ni Mwajuma Juma (ZPC), Imane Duwe (SUZA) na Shifaa Said (MCT - Z'BAR).
Comments
Post a Comment