SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

Samia ataka wadau kutathmini mafanikio yaliyofikiwa

  • Asema agenda ya usawa wa jinsia inahitaji mashirikiano
  • Aipongeza FAWE kuchochea kasi ya maendeleo ya elimu

NA MWANDISHI WETU

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewataka wadau wa masuala ya jinsia nchini kuitumia siku ya kimataifa ya wanawake duniani kufanya tathmini na kuweka mikakati ya kusukuma mbele agenda ya maendeleo ya jinsia badala ya kulalamika.

Ameeleza kuwa kufanya hivyo kutachochea kasi ya mendeleo ya wanawake duniani kwani siku hiyo inatoa fursa kwa serikali, taasisi zisizo za serikali na wadau kupima utekelezaji wa harakati za kumjengea uwezo na kumkomboa Mwanamke na mtoto wa kike.

Makamu wa Rais alieleza hayo juzi usiku katika harambee iliyoandaliwa na Jumuiya ya kuwawezesha wanawake Zanzibar (FAWE) ikiwa ni sehemu ya madhimisho ya siku ya wanawake duniani inayofikia kilelele chake leo, iliyofanyika hoteli ya Serena mjini Unguja.

Alisema ili kuhakikisha mwanamke na mtoto wa kike anakuwa na sauti katika jamii na taifa kwa ujumla, wadau hawana budi kushirikiana ili kuhakikisha maendeleo yao katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii yanafikiwa.

 “Sote ni mashahidi kuwa karne hii ya 21 ni karne ya sayansi na teknolojia inayoendeshwa na mapinduzi ya viwanda. Sasa ili sote tuweze kunufaika na fursa mbali mbali za mapinduzi haya lazima tushirikiane ili kuhakikisha hakuna kundi linaloachwa nyuma katika safari ya maendeleo,” alisema Samia.

Aidha aliipongeza FAWE kwa kuendelea na wajibu wa kumpigania mwanamke kwa miaka 23 tangu kuanzishwa kwake na kuwa chachu ya kuhakikisha kuwa wanawake na watoto wa kike wa Zanzibar wanapata haki zao za msingi za elimu, uchumi na haki za kijamii kwa usawa.

Alieleza kupitia programu mbali mbali, FAWE wamesaidia wanafunzi wa kike zaidi ya 3,000 kutoka kwenye kaya maskini kufikia malengo ya kupata elimu toka mwaka 2001 hadi sasa.

Samia aliongeza kuwa kuna umuhimu mkubwa wa wanafunzi wa kike kujikita katika masomo ya sayansi na teknolojia ili kuzalisha wataalamu wa kike watakaoweza kutumikia uchumi wa viwanda katika sekta mbali mbali.

Alisema kwa upande wa Zanzibar, Serikali inajipanga kujikita kwenye masuala ya uchumi wa bluu unaohusisha sekta za mafuta na gesi, kilimo cha mwani, uvuvi wa bahari kuu na uvuvi wa vizimba ambazo zitaimarisha kasi ya ujenzi wa viwanda vitakavyoongeza thamani mazao ya baharini.

“Mtoto wa kike hadi leo bado anakabiliwa na vikwazo mbali mbali ikiwemo mila potofu, ndoa za umri mdogo na majukumu ya nyumbani na jambo la kusikitisha kwamba bado tunaendelea kulalamika tu bila kuchukua hatua tiba za tatizo hilo,” alisema.

Aliongeza kuwa serikali inaendelea kutoa elimu bure katika ngazi ya maandalizi, msingi pamoja na kuimarisha mafunzo ya amali na elimu ya juu, sambamba na kuimarisha hali ya skuli na kurejesha masuala yanayotakikana ili watoto kusoma na kufaulu masomo ya sayansi.

Aidha Samia alieleza kwa kipindi cha miaka tisa, bajeti ya sekta ya elimu imeongezeka kwa asilimia 91.4 kutoka shilingi 93,468,089,000 mwaka 2010/2011 hadi kufikia shilingi 178,917,149,000 mwaka 2019/2020 jambo linalothibitisha utayari wa serikali kuwekeza katika elimu.

“Ongezeko la bajeti limesaidia kuendeleza miundombinu ya elimu na kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia, kuweka vituo maalum vya masomo ya sayansi, kuongeza idadi ya walimu, vitendea kazi ikiwemo vitabu pamoja na kuanzishwa skuli za watoto wa kike peke yao (skuli ya Benbella),” alisema Makamu wa Rais.

Awali Waziri wa  Elimu na Mafunzo ya Amali (WEMA), Simai  Mohamed  Said, alisema jumuia hiyo inaendelea kujitolea kuhakikisha mtoto wa kike anakuwa mstari wa mbele kuleta maendeleo ya taifa.

Alisema katika kuhakikisha mtoto wa kike anapata taaluma za ujasiriamali kwa lengo la kuhakikisha taifa linakuwa na vijana wasomi na shupavu katika nyanja zote jumuiya hiyo mekuwa ikishirikiana na wizara yake kufanikisha ndoto za wanafunzi na walimu.

Nae Mwenyekiti wa FAWE Zanzibar, Dk. Mwatima Abdalla Juma, alisema wamekuwa mstari wa mbele kumuinua na kumuendeleza mtoto wa kike, sambamba kuwahamasisha ushiriki wa mwanamke katika uchumi kwa njia ya kuelimisha na kuwapatia fursa mbali mbali za kujiendeleza kiuchumi.

Alisema kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu Zanzibar, wamefanikiwa kuwarejesha watoto wa kike masomoni baada ya kukata tamaa ya kuendelea na masomo kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo za kiuchumi.

Akitoa ushuhuda kwa niaba ya wanafunzi wenzake, mmoja ya wanufaika wa program za jumuiya hiyo, Amina Omar Kitwana, kutoka kijiji cha Matemwe, mkoa wa kaskazini unguja, alisema FAWE imewasaidia kurudi masomoni na kujifunza kazi mbali mbali za ujasiriamali ambazo zimewasaidia kuleta maendeleo kwa familia zao.

Siku ya kimataifa ya wanawake dunia, huadhimishwa kila ifikapo Machi 8, ya kila mwaka ambapo katika harambee hiyo, zaidi ya shilingi milioni 32 zilikusanywa kama fedha taslimu na ahadi.

 

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango