Soraga ahimiza mafunzo kwa watendaji kuongeza ufanisi
NA SHARIFA MAULID, WNARKUU
WAZIRI wa Nchi Afisi ya Rais, Kazi, Uchumi na
Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga, ametilia mkazo suala la kupatiwa mafunzo
wafanyakazi ili kuwajengea uwezo wa utakaoimarisha utendaji katika maeneo yao.
Ameeleza hayo wakati akizungumza na wafanyakazi
wa Idara ya Utumishi na Uwendeshaji ya wizara hiyo juu ya utekelezaji wa
majukumu yao katika ukumbi wa wizara
yake Mwanakwerekwe, wilaya ya Magharib ‘B’.
Alisema katika utekelezaji wake, Wakurugenzi wa
idara hiyo waangalie mahitaji na sio kupewa mtu mmoja kila inapotokea nafasi za
mafunzo ili kuondosha manung’uniko miongoni mwa wafanyakazi.
Soraga aliwataka viongozi na wafanyakazi kufuata
taratibu za kazi, muongozo wa sheria za
kazi na maagizo yanayotolewa na serikali kwa lengo la kuweka mustakabali mzuri
utaopelekea ufanisi wa majukumu ya kila
mmoja na maendeleo ya wananchi kwa ujumla.
Hivyo aliutaka uongozi wa Idara hiyo kuhakikisha
wafanyakazi wanapatiwa stahiki zao, kupandishwa madaraja na kuweka mfumo mzuri
utakaoweka wazi kujua muda wa kuingia na kutoka kazini kuimarisha nidhamu
kazini.
“Tukiweza kufanikisha haya, sina shaka tutafika mbali
na kwa ufanisi kwani sisi sote tunafanyakazi moja, tushirikiane, tuwe na
mawasiliano mazuri na kuzidisha umoja wetu,” alisema Mudrik.
Aidha Soraga alisisitiza haja ya kutumiwa
kikamilifu anuani za barua pepe za wizara katika mawasiliano ya kikazi badala
ya kutumia barua pepe binafsi kwani kufanya hivyo kunavujisha taarifa za
serikali.
“Hakikisheni wafanyakazi wote mnawapatia email
zao za Wizara hili si ombi ni amri, tuna mambo mengi ya serikali, sasa kutumia
e-mail (barua pepe) binafsi, hii ni kurahisisha uvujaji wa taarifa za
serikali,” alieleza waziri huyo.
Katika hatua nyengine, Soraga aliwataka watendaji
wa idara hiyo kuwa makini katika utendaji wa kazi zao na kukemea tabia ya baadhi
ya watumishi kuondoka kazini kabla ya wakati.
Kuhusu wakurugenzi wa Idara zilizomo katika
wizara yake, Soraga aliwataka kutumia vyombo vya habari wanapofanya shughuli
zao ili wananchi wajue serikali inayoyafanya.
Comments
Post a Comment