TASAF kujenga wodi ya akina mama, maabara zahanati ya Mkambarani
NA JAMES MWANAMYOTO, MOROGORONAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Deogratius Ndejembi, (pichani) ameiahidi Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Utawala na Serikali za Mitaa, kwamba kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) serikali itajenga wodi ya
kuwahudumia akina mama wajawazito na maabara katika zahanati ya kijiji cha Mkambarani
ili wananchi hao wapate huduma bora za afya.
Ndejembi ametoa ahadi hiyo ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya
kamati hiyo iliyoelekeza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kujenga jengo la
kina mama kwa ajili ya kuwapatia huduma stahiki, ikiwa ni pamoja na kujenga
maabara itakayotoa huduma bora na vipimo wananchi wa Mkambarani.
Amesema, kutokana na maelekezo yaliyotolewa na kamati ofisi yake
itajenga wodi ya akina mama ili kuwe na faragha wakati wa kuwahudumia akina
mama wajawazito.
Kuhusu maelekezo ya ujenzi wa maabara, Ndejembi ameihakikishia
kamati na wananchi wa kijiji hicho kwamba maabara itakayojengwa itawaondolea
adha wananchi hao ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma na kuingia gharama
kubwa.
Ameongeza kuwa, lengo la serikali kujenga zahanati ya Mkambarani
ni kuwasogezea karibu huduma za afya wananchi wa eneo hilo ikizingatiwa kuwa,
walengwa wa TASAF watanufaika pia na huduma zinazotolewa na zahanati hiyo na
hatimaye kuwa na afya bora itakayowawezesha kupambana na umaskini kupitia
ruzuku ya TASAF wanayoipata.
Akitoa maelekezo kwa serikali kwa niaba ya kamati yake, Mwenyekiti
wa Kamati hiyo Humphrey Polepole, amesema Kamati imelazimika kutoa maelekezo ya
ujenzi wa Wodi ya akina mama na maabara kama sehemu ya kulinda utu wa wananchi
hususani akina mama wanaofuata huduma ya uzazi katika zahanati ya Mkambarani.
Aidha Polepole amesema,
wodi ya akina mama ikijengwa itaongeza usiri na faragha wakati wa kuwahudumia
wajawazito tofauti la ilivyo sasa ambapo hakuna usiri wa kutosha wala faragha
pindi akina mama wanapohudumiwa.
Kuhusiana na maelekezo ya ujenzi wa maabara, Polepole ameeleza
kuwa, kamati yake imepata fursa ya kuitembelea zahanati ya Mkambarani na
kubaini kuwa hakuna maabara inayokidhi mahitaji ndio maana kamati yake
imeielekeza Serikali kujenga maabara itakayokidhi kutoa huduma stahiki kwa
wananchi wa kijiji cha Mkambarani.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa imemaliza ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Dar es Salaam, Pwani na Morogoro iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Picha na maelezo yake:


BAADHI ya wananchi wa Kijiji cha Mkambarani, Morogoro
wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za
Mitaa, Humphrey Polepole (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya kamati
hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF kijijini hapo.
Comments
Post a Comment