UNDP kushirikiana na SMZ kuendeleza miradi ya uchumi
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nchi Afisi ya Rais Fedha
na Mipango, Jamal Kassim Ali (pichani), amefanya mazungumzo na Mwakilishi Mkaazi wa
Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja
wa Mataifa (UNDP), Christine Musisi na kujadiliana namna shirika hilo litakavyosaidia
miradi ya maendeleo ya kukuza uchumi wa Zanzibar.
Mazungumzo hayo yamefanyika jana,
katika Ofisi ya Uratibu wa Shughuli za SMZ zilizopo katika ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais, jijini Dar es Salaam.
Jamal alisema Serikali ya Mapinduzi
Zanzibari itaendelea kushirikiana na washirika wa maendeleo wa ndani na nje
ikiwemo UNDP, kusaidia uwajibikaji na utendaji kazi wa serikali kwa ufanisi
kama alivyoagiza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar
wa awamu ya nane Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Alisema Zanzibar imejipanga katika
kuimarisha uwajibikaji na utendaji kazi kwa wafanyakazi wake ili kuhakikisha
nchi inafikia malengo yaliyowekwa wa uchumi wa buluu.
Aliongeza kusema kwamba, shirika hilo
litasaidia katika uchumi wa buluu katika kuandaa sera na kujengea uwezo
watendaji katika fani mbali mbali ili kufikia azma hiyo ya serikali.
Alifafanua kuwa, UNDP imeweka nguvu
zake katika kusaidia Baraza la Wawakilishi la Zanzibar vifaa vya kisasa na
kuwajengea uwezo ili liendane na mfumo wa mawasiliano wa sayansi na teknolojia
pamoja na kuzijengea uwezo Halmashauri za Zanzibar kivifaa na kiutendaji.
Sambamba na hilo wataendelea
kuimarisha mahakama za Zanzibar kwa kuvipatia nyezo za kufanyia kazi kwa
ufanisi na kwa haraka zaidi katika kutoa maamuzi.
Jamal alieleza kuwa Dk. Mwinyi, ameruhusu
kuanzishwa kwa mahakama maalumu ya udhalilishaji wa watoto na wanawake ili
kupambana na kuondosha masuala hayo katika jamii.
Comments
Post a Comment