Vijana watakiwa kutumia vyema mitandao ya kijamii

NA MADINA ISSA

MKURUGENZI Mtendaji wa Jumuiya wa Jukwaa la Vijana Zanzibar Zanzibar Youth Forum (ZYF), Maulid Suleiman, (pichani aliesimama) amewataka vijana nchini kutumia mitandao ya kijamii ipasavyo, ili kuepusha kuleta athari kwa mbalimbali kwa jamii.

Maulid alitoa wito huo jana wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana kupitia mradi wa kukuza ushiriki wa asasi za kiraia katika sheria na uhuru wa msingi wa vyombo vya habari, yaliyofanyika katika ukumbi wa kitengo cha kudhibiti malaria Mwanakwerekwe Mjini Unguja.

Alisema vijana wengi wanatumia vibaya mitandao hiyo na kusababisha migogoro ndani ya jamii.

Alisema ni vyema kwa vijana hao kutumia mitandao hiyo kwa kutoa taarifa sahihi ambazo zitaleta mafanikio nchini na kufikia malengo yaliyokusudiwa ikiwemo kuelimisha jamii hasa wanaotumia mitandao ya kijamii.

Aidha alisema kuwa lengo la mradi huo ni kuwajengea uwezo taasisi zisizo za kiserikali na ushiriki na utetezi juu ya sera za habari, uhuru wa habari na haki za msingi za binaadamu.

Akiwasilisha mada ya matumizi ya mazuri ya mitandao, Mwanahabari Mwandamizi, Dk. Suleiman Seif Omar, alisema wapo baadhi ya vijana hutumia mitandao ya kijamii kwa kuandika taarifa bila ya kufuata sheria jambo ambalo linaweza kuleta vurugu na sintofahamu katika nchi.

alisema kupatiwa mafunzo hayo kutawawezesha kutangaza habari zilizokuwa na ubora na za kweli kwa lengo la kuielimisha jamii.

“Sasa hivi kila mtu ni muandishi wa habari watu wanaitumia taaluma hii wanavyotaka hivyo ni vyema vijana wakaacha mtindo huu kwani uandishi wa habari ni taaluma na unatakiwa usome na kujua taratibu za kupasha habari na sio uvamie tu,” alisema.

Hivyo, alisema ni vyema wakatumia taratibu na sheria za mitandao ya kijamii kwa kuandika taarifa bila ya kumkwaza mtu kwa kutuma picha sahihi na taarifa zilizokuwa sio za uongo ambazo zitakuwa zimefanyiwa tafiti wa kina ili kuweza kufaidia juu ya habari atakayoituma.

Nao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, walisema mafunzo hayo yatawasaidia kujua sheria za mitandao na kutoa taarifa sahihi kupitia mitandao au mawasiliano yao ya kawaida.

Walisema ipo haja kwa asasi za kiraia kutumia mitandao ya jamii kuimarisha upatikanaji wa habari kwa jamii ili kustawisha maendeleo ya nchi na watu wake.

Mradi huo wa miaka miwili, unatekelezwa na ZYF chini ya ufadhiliwa na shirika la International Media Support (IMS) la Denmark chini ya uangalizi wa MISA TAN, UTPC na TAMWA umelenga kuimarisha matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na kuongeza uelewa wa wanachama wa asasi za kiraia juu ya sheria zinazohusiana na vyombo vya habari.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango