Waziri ataka wanawake kuinua sekta
ya utalii
NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Utalii na Mambo ya Kale,
Lela Mohammed Mussa, amewataka wanawake kuungana kuitetea jinsia yao na kuachana
na mila za kuamini kuwa kufanya kazi katika sekta ya utalii kwa wanawake ni
kinyume na utamaduni.
Akizungumza katika hafla ya maadhimisho
ya siku ya wanawake duniani Machi 8, mwaka huu iliyoandaliwa na hoteli ya Park
Hyatt, ikiwa na lengo la kuwahamasisha wanawake kuunga mkono katika shughuli
mbali mbali zikiwemo za kisiasa na kijamii.
Alisema jamii ya Wazanzibari imekuwa
ikitawaliwa na dhana mbaya kuhusiana na sekta hiyo kiutalii lakini jamii hiyo
ya wanawake inajitambua na imeonekana kufanya vizuri katika ajira mbali mbali bila
ya kuharibu mila, silka, desturi na tamaduni zao.
Aidha alisema utafiti uliofanyika duniani
unaonesha kuwa dhamana nyingi walizopewa wanawake kuzifanyia kazi wamekuwa
wakifanya vizuri zaidi kuliko wanaume.
Hivyo, alisema kuwa hakuna haja ya
kuendelea kuvunjana moyo na badala yake wawe kitu kimoja hasa Katika kuendelea
kuleta mabadiliko Katika nchi.
Naye Meneja Mkuu wa hoteli ya Park
Hyyat, Nicolas Cedro, alisema hoteli hiyo inathamini utendaji wa kazi kwa
jinsia ya kike kwani wamekua na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi.
"Katika hoteli yetu tumekuwa
tukithamini sana wanawake, kwani wana mchango mkubwa sana katika kufanya kazi
na siye tutaendelea kuwathamini na kujua umuhimu wa kazi zao wanazozifanya,"
alisema.
Mapema Mejeja Rasilimali watu katika
hotel hiyo, Catherine Msuya, alisema atahakikisha wanaongeza nafasi kwa wanawake
ambao kwa sasa ni zaidi ya asilimia 20 ya wafanyakazi wote hotelini hapo.
PICHANI:
WAZIRI
wa Utalii na Mambo ya Kale, Lela Mohammed Mussa akipokea cheti cha shukran
kutoka kwa Meneja Mkuu wa hoteli ya Park Hyyat
Nicolas Cedro Wakati wa
sherehe za maadhimisho ya siku wa wanawake Machi 8 mwaka huu. Wa kwanza kulia
ni afisa rasili mali watu wa hoteli hiyo,
Catherine Msuya. (PICHA NA
MZEE GEORGE).
Comments
Post a Comment