Zanzibar  yaadhimisha siku ya ustawi kimataifa kwa mara ya kwanza

  •  Maafisa ustawi, wadau watakiwa kuzingatia maadili

NA KHAMISUU ABDALLAH

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesema inathamini juhudi na mchango unaotolewa na maofisa ustawi wa jamii katika kusaidia jamii iliyowazunguka.   

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed, katika hotuba yake ya kilele cha maadhimisho ya ustawi duniani iliyotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa wilaya Magharibi ‘A’, Suzan Peter Kunambi, katika ukumbi wa shekh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Machi 16 mwaka huu.

Maadhimisho hayo yanayofanyika kila Jumanne ya tatu ya mwezi wa tatu, Masoud alisema serikali  itaendelea kuwashika mkono na kutambua mchango wa Maafisa ustawi wa jamii kwani ni watu muhimu katika jamii.

Alisisitiza kwamba serikali imelenga kuimarisha ustawi wa wananchi wa Zanzibar kama yalivyokuwa madhumuni ya mapinduzi ya Zanzibar.

Alibainisha kuwa serikali ya awamu ya nane  inayoongozwa na  Dk. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,imedhamiria kuinua maisha ya Wazanzibari katika kila nyanja ikiwemo kisiasa, kijamii na kiuchumi.

“Katika kuthibitisha hili, mnaziona juhudi zinazochukuliwa na serikali yetu toka awamu ya kwanza kuwatunza na kuwalinda wazee kwa kuthamini mchango walioutoa katika nchi yao ikiwemo kuwapa pencheni kila mwezi,” alisema.

Alisema pia serikali imeanzisha sheria namba 2 ya mwaka 2020 yenye lengo la kuimarisha ustawi wa wazee hapa Zanzibar.

Kwa upande wa watoto alisema serikali imefanya jitihada mbalimbali za kuimarisha ustawi wa watoto kwa kuanzisha sera, sheria na kanuni ili kuwalinda kuwafanya kuwa na vijana bora katika taifa.

Alisema ni jukumu kwa wanaustawi kutumia taaluma zao ipasavyo katika kuisaidia jamii na kuisaidia mipango inayopangwa na serikali kwani kufanya hivyo itakuwa wametimiza wajibu wao ipasavyo.

Mbali na hayo, alisema katika makundi hayo pia kuna watu wenye ulemavu hivyo ni kazi kwa wanaustawi hao kuangalia ustawi wa watu hao kwani wana mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi yao.

Aliwapongeza wanaustawi hao kwa kazi kubwa na ya wito wanayoifanya katika jamii hivyo ni vyema kazi hiyo wakaifanya kwa uadilifu, uzalendo na upendo.

Mbali na hayo alizipongeza jumuiya mbalimbali zinazotoa mchango katika suala la ustawi wa jamii na kuwaomba kuendelea kuisaidia serikali kuimarisha ustawi wa jamii hasa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.

Akizungumzia suala la udhalilishaji, alisema ni wajibu wana ustawi wa jamii kuisadia serikali katika mapambano hayo kwani kufanikiwa kwa mahakama ya udhalilishaji kunategemea sana ushahidi. 

“Tunamuona Rais wetu anavyokerwa na vitendo vya udhalilishaji na ndio maana katika kuona haya yote yanafanikiwa kaanzisha mahakama ya kesi hii andaeni mradi wa kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kutoa ushahidi na ushirikiano pale kesi zinapofikishwa mahakamani,” alisisitiza.

Naibu Katibu Mkuu, wizaya ya Afya, Uatawi wa Jami, Wanawake na Watoto, Jamii Abeda Rashid Abdalla, alisema siku ya ustawi ni muhimu katika kusimamia masuala ya ustawi wa jamii nchini.

Aliwasisitiza kutojisahau katika kazi wanazozifanya kwa kushirikiana pamoja katika kuona ustawi wa wazee na watoto unaendelea kuimarika.

Mbali na hayo aliwaomba wana ustawi na watoa huduma katika maeneo mbalimbali ya kijamii ikiwemo hospitali, kuhakikisha wanatoa vipaumbele kwa wazee kwani nao wanahitaji malezi kama ilivyo kwa watoto na watu wengine wenye mahitaji.

Akisoma risala kwa niaba ya maofisa ustawi wa idara taasisi za serikali na zisizo za kiserikali, Selwa Ali Sheha, alisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutotambuliwa kwao, kukosa ajira na vitendea kazi katika kufatilia kesi ikiwemo usafiri.   

Siku ya Ustawi wa Jamii huadhimishwa kila ifikapo Machi 16 ya kila mwaka ambapo ujumbe wa mwaka huu; ‘Mimi nilivyo unatokana na sisi tulivyo tuimarishe mshikamano wa jamii na uhusiano wa ulimwengu’.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango