ZPC yaomboleza kifo cha JPM

NA MZEE GEORGE

WAKATI mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, marehemu Dk. John Magufuli ukifikishwa katika kijiji chao cha Chato mkoani Geita, wananchi na viongozi wa ngazi mbali mbali wamejitokeza kusaini vitabu vya maombolezo vilivyowekwa katika maeneo mbali mbali nchini.

Miongoni mwa wananchi na viongozi  waliofanya hivyo jana ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, alieweka saini katika vitabu hivyo vilivyowekwa katika Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar Kisiwandui na ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil.

Kwa upande wa viongozi wa asasi za kirai, Katibu Mkuu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar, Mwinyimvua Nzukwi ambae aliweka saini katika vitabu hivyo Machi 24, 2020  na kueleza kusikitishwa kwao na kifo hicho.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Nzukwi alieleza kuwa kifo cha Dk. Magufuli ni pigo na kwamba kimeacha pengo katika ujenzi wa taifa.

Alieleza kuwa Dk. Magufuli licha ya kuwa ni kiongozi wa kitaifa, bado alikuwa mdau na chanzo muhimu cha habari na kuvipongeza vyombo vya habari kwa kuungana na kutoa taarifa za matukio ya kifo cha kiongozi huyo.

Alisema toka kutokea kwa msiba huo, vyombo vya habari vimekuwa vikitoa taarifa na uchambuzi wa habari uliowawezesha watanzania na walimwengu kuwa na uelewa jambo lilisaidia kuongeza umoja na mshikamano kama taifa.

Akizungumzia hatua ya kusaini kitabu hicho alisema kunatokana na kuguswa kama mwananchi lakini kiongozi wa taasisi inayowaunganisha waandishi, waliona umuhumu wa kuonesha kuhguswa kwao na kifo cha kiongozi huyo aliefariki Machi 17, 2021 katika hospitali ya Mzena jijini Dar es salam.

“Hakika umeondoka wakati sote tukikuhitaji, pumzika kwa amani. RIP – JPM,” aliandika Nzukwi katika kitabu cha CCM na “Waandishi wa habari na Wanachama wa Klabu za Wanahabari zitakumbuka mchango wako katika ujenzi wa taifa siku zote, RIP – JPM,” katika kitabu cha serikali.

Maziko ya Dk. Magufuli yanatarajiwa kufanyika machi 26, 2020 kijijini kwao chato, mkoani Geita ambapo mwili wa kiongozi huyo ulifikishwa kijijini hapo Machi 24, 2021 majira ya saa 12:30 jioni ukitokea Zanzibar ambapo uliagwa Machi 23 kabla ya kuagwa Mwanza asubuhi ya Machi 24, 2021.

Pichani na maelezo:

KATIBU Mkuu wa ZPC Mwinyimvua Nzukwi, akisaini kitabu cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, marehemu Dk. John Pombe Magufuli, katika Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar, Kisiwandui, Zanzibar.

KATIBU Mkuu wa ZPC Mwinyimvua Nzukwi, akisaini kitabu cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, marehemu Dk. John Pombe Magufuli, katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, Kikwajuni Zanzibar. (PICHA NA MZEE GEORGE).


 

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango