Sakata la kupigwa mwandishi Z'bar: SMZ yaahidi kuchukua hatua kwa waliohusika

  • Wadau wasema ni mwanzo mzuri, waahidi kuendelea kufanya kazi nayo

NAMWANDISHI WETU

SIKU moja baada ya kutokea tukio la udhalilishaji wa mwanahabari Jesse Mikofu wa gazeti la Mwananchi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, imeahidi kuwachukulia hatua askari wanne wa Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ) wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo.

Jesse alishambuliwa na askari hao waliokuwa wakiwaondoa wafanyabiashara wadogo wadogo (wamachinga) katika eneo la Darajani, mjini Unguja, akiwa anatekeleza majukumu yake ya uandishi wa habari.

Akizungumza mkutano wa pamoja wa Waandishi wa habari, ulioitishwa kwa pamoja na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Tabia Maulid Mwita na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed, kwa ajili ya kutoa tamko la serikali, uliofanyika katika ofisi za Wizara ya Habari, Migombani.  

Masoud, alisema serikali ya Zanzibar inaendeshwa kwa kuzingatia misingi ya haki, uadilifu, kama inavyoelekeza katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na sheria nyengine, hivyo haikuridhishwa wala kukubaliani na tukio hilo.

Aliongeza kuwa tukio hilo ni ukiukwaji wa taratibu za utekelezaji wa kazi za vikosi hivyo na kwamba itahakikisha inachukua hatua kwa mujibu wa sheria kwa wote waliohusika na tukio hilo.

“Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaungana na wadu wengine wa habari na haki za binadamu kulaani tukio hilo kwani sio maagizo wala maelekezo walilyopewa na sio utamaduni wa chombo chochote cha ulinzi bali ni tukio lilofanywa na watu wasiokuwa na maadili ya kazi na kutotambua mipaka ya shughuli zao,” alieleza Masoud.

Alibainisha kwamba mbali ya kufanya mawasilianao na muhisika (Jesse), amemuagiza Kamanda Mkuu wa KVZ, ahakikishe anatoa orodha ya watendaji waliokuwepo katika eneo la Darajani siku ya tukio ili kuwabaini waliofanya udhalilishaji huo kwa hatua zaidi za kisharia na kinidhamu.

“Walipokuwa katika majukumu yao ya kazi, hawakupaswa kukiuka kwa haki au kuzuwia watu wengine wasitekeleze majukumu yao, kwani waandishi walikuwa na haki ya kutekeleza wajibu wao kama ilivyokuwa kwao,” alibainisha.

Alisema utekelezaji wa majukumu ya vikosi hivyo unasimamiwa na sheria hivyo serikali itahakikisha hatua zinachgukuliwa ikiwa ni pamoja wahusiika kupelekwa katika mahkama za kijeshi.

Aidha Masoud mbali ya kukiri kuwa vikosi hivyo vimekuwa vikitenda matendo ya ukiukwaji wa haki za wengine mara kwa mara, alisema hatua ,mbali mbali zitachukuliwa kwani kufanya hivyo ni utovu wa nidhamu wa baadhi ya watendaji wa taasisis hizo na kuwahakikishia wanahabari kuwa tukio kama hilo haliwezi kujirejea.

“Tukio hili tunataka liwe kigezo cha kuona jinsi vikosi vyetu vinavyotekeleza majukumu yao kwa kuheshimu misingi ya kazi zao lakini pia haki za wengine wakiwemo wanahabari hivyo msiwe na hofu mnapotekeleza majukumu yenu,” alieleza Masoud.

Nae, Waziri wa Habari Vijana, Utamaduni Sanaa na Michezo, Tabia Maulid Mwita, alitoa pole kwa Mwandishi huyo na tasnia ya habari kwa ujumla na kueleza kwamba Zanzibar itaendelea kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa vyombo hivyo.

Alisema, wizara inachukua juhudi mbalimbali kuhakikisha wanahabari wanapata haki zao na kutatua changamoto zao ili kuona wanahabari wanafanya kazi katika mazingira mazuri.

Aidha aliwahakikishia Wanabari kuwa Wizara yake itaendelea kuwalinda , kulinda maslahi yao na kuweka mazingira mazuri ya kufanyia kazi zao na kutoa pole kwa mwandishi huyo huku akiahidi kumlinda na kuilinda tasnia ya habari aliydai kuwa ni chombo muhimu cha kuunganisha nchi.

"Kama nilivyopata kusema awali, serikali haitokubaliana na vitendo vyovyote vinavyoathiri uhuru wa habari kwa kutambua kuwa tasnia hii ndio daraja linaloiunganisha Zanzibar na nchi nyengine lakini pia ni chombo kinachochea maendeleo ya nchi na watu wake," aliongeza Waziri Tabia.

Kwa upande wake Katibu Mkuu  wa Klabu ya Waandhishi wa habari Zanzibar (Zanzibar Press Club) Mwinyimvua Abdi Nzukwi, alieleza kuwa kwa kushirikiana na Muungano wa Klabu za Wanandishi wa Habari Tanzania (UTPC), ilistushwa na tukio hilo ambalo linahujumu uhuru wa habari lakini pia kuleta athari mbaya kwa taifa katika maswala ya uhuru wa habari kimataifa.

Alisema swala la uhuru wa habari ni nyeti na linalogusa hisia za wengi, hivyo kunaumuhimu wa kila mmoja miongoni mwa jamii kuzingatia hilo ikiwa ni pamoja na kuzingatia mipaka, misingi na utaratibu zilizopo wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Hata hivyo alishukuru na kupongeza hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia mawaziri hao na kuitaja kuwa inaonesha kuwa serikali ina nia ya dhati ya kukuza uhuru wa habari na wa kujieleza nchini.

“Bahati mbaya sana tukio hili limekuja wakati dunia inaelekea kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya kimataifa ya uhuru wa habari Mei tatu mwaka huu, kimsingi limetia doa lakini hatua zilizochukuliwa zinatia moyo na tunaamini hatua zitakazoichukuliwa zitasaidia kuimarisha mahusiano kati ya serikali na vyombo vya habari,” alieleza Nzukwi.

Mapema asubuhi akizungumza katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja, Mwandishi aliepatwa na madhila hayo, Jesse Mikofu, alisema hakuna mtu yoyote aliyekuwa juu ya sheria hivyo ni vyema vikosi hivyo kufuata sheria zilizowekwa badala ya kuchukua hatua mikononi pale mtu inapotokea amevunja sheria.

“Nilichofanyiwa mimi ni udhalilishaji kwani walinitesa kiasi kile wakati nilikuwepo kwenye kazi na niliwaonesha vitambulisho vyangu lakini waliamua kunidhalilisha kwa kunigaragaza kwenye maji na kunipiga,” alisema.

Akizungumzia hali yake ya kiafya, alisema anaendelea vizuri lakini bado ana maumivu katika sehemu mbali mbali za mwili, ikiwemo kwenye bega, mguu, mkono, mgongoni na ubavu katika sehemu ya kushoto na nyayo za miguu.

Akitoa salamu za wanahabari wakati wa mkutano wa Mawaziri hao, mwandishi Farouk Kareem wa ITV, aliipongeza serikali kwa kuchukua hatua ambayo imewapa moyo wanahabari juu ya tukio hilo.

Alisema jamii ya wanahabari imeridhika na hatua iliyochukuliwa na kuahidi kuendelea kufanya kazi kuisadia serikali kutangaza maendeleo ya Zanzibar na kumuomba Waziri anaehusika na vikosi, kuvipatia mafunzo na kuwapa elimu watendaji wakejuu ya uadilifu, ulinzi wa haki za binadamu na uhuru wa habari wanapotekeleza majukumu yao.

Mwandishi wa habari wa Mwananchi Communication Limited (Zanzibar), Jesse Mikofu, alipatwa na kadhia hiyo April 21 mwaka huu, katika maeneo ya Vikokotoni mjini Unguja akiwa kazini baada ya kupiga picha askari waliokuwa wakiwaondosha wafanyabiashara wadogo wadogo katika maeneo hayo na kupata majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.

PICHANI: WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum ya SMZ, Masoud Mohammed Ali (kushoto), akitoa tamko la serikali kuhusiana na tukio la kudhalilishwa kwa Mwandhishi wa Habari wa kampuni ya Mwananchi Communication, Jesse Mikofu na askari wa Kikosi cha Valantia (KVZ) Aprili 21, 2021 katika maendeo ya Darajani, Zanzibar. Kulia ni Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Tabia Maulid Mwita.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango