SUK tunda la maridhiano linalopaswa kuenziwa

• Vyombo habari, NGOs zatajwa kuchangia uimara wake

NA ASYA HASSAN
KUWEPO kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ya Zanzibar inayoundwa na vyama vya CCM na ACT Wazalendo, kunatajwa kuwa ni matokeo ya maridhiano ya kisiasa yaliyolenga kutatua mgogoro wa kisiasa wa muda mrefu ulioikumba Zanzibar.
Mgogoro huo unatajwa kusababisha mifarakano ya kijamii na kuzorotesha maendeleo ya kijamii sambamba na kudhoofisha maswala ya amani na utulivu hasa baada ya kurudishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania.
Mfumo huo uliorudishwa mwaka 1992, ulianza kuonesha dalili za misuguano na mifarakano katika jamii hata kabla ya uchaguzi wa kwanza wa mwaka 1995 ambao ulikuwa na ushindani mkali kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).
Yapo mambo mengi yaliyoashiria uvunjifu wa amani wakati wa uchaguzi huo na hata katika chaguzi nyengi zilizofuata kabla ya uchaguzi mkuu wa 2010 ambao ndipo chimbuko la maridhiano ya kisiasa Zanzibar lilitamalaki.
Pamoja na ushindani uliokuwepo, bado Chama cha Wananchi (CUF) kupitia mgombea wake marehemu maalim seif sharif hamad, alikubali matokeo ya uchaguzi huo na kushirikjiana na mgombea wa ccm dk. Ali Mohamed shein kuunda serikali.
Hali hiyo ilisaidia kupunguzamekuja baada ya visiwa hivi kutoka katika uchaguzi mkuu uliyovihusisha vyama mbalimbali vya kisiasa na kuwafanya wananchi kutofautiana kwa namna moja au nyengine kutokana na mihemko ya kisiasa.
Hivyo kutokana na hali hiyo ndipo serikali ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Hussein Ali Mwinyi, ulipofuata katiba na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kutokana na kuamini kwamba kufanya hivyo ndio mwarubaini wa kuondosha tofauti za wananchi na kuwafanya kuwa kitu kimoja.
Mbali ya serikali kutaka nchi kuwa na amani kwa kuamini kwamba wananchi wanahitaji maendeleo na asasi zisizo za kiserikali nazo zimekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono serikali.
Katika kutekeleza majukumu yao, asasi hizo zinatajwa kuwa na mchango mkubwa katika hali iliyojitokeza kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa oktoba 28 mwaka uliopita.
“Kama wadau wa maendeleo lakini pia amani ya nchi yetu, tulifanya juhudi za kuwanasihi wananchi hasa makundi ya vijana kudumisha amani na utulivu ili kuweza kufikiwa kwa malengo ya serikali ya kuleta maendeleo ya haraka kwa wananchi wake,” anaeleza Maulid Suleiman, mkurugenzi wa Zanzibar Youth Forum (ZYF).
Alieleza kuwa kupitia programu mbali mbali na kushirikiana na asasi nyengine zinazohusiana na vijana walitoa mafunzo juu ya njia bora ya kutunza amani kama chachu ya maendeleo ya jamii.
Akizungumzia mchango wa vyombo vya habari katika kustawisha amani, umoja na maelewano wakati wa mchakato wa uchaguzi, mwenyekiti wa Klabu ya ya waandishi wa habari Zanzibar (ZPC), Abdalla Abdulrahman Mfaume, alieleza kuwa walihamasisha waandishi kufanya kazi zao kwa kuzingatia weledi, sheria na kanuni hatua ambayo imesaidia kudumisha amani na utulivu.
Alisema klabu hiyo pia imekuwa ikiwasisitiza waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika kuwasisitiza wananchi kuridhia kwa serikali iliyoundwa na kilichobaki ni kutekeleza majukumu yao ili kuona maendeleo yanapatikana kwa haraka.
Anasema sekta ya habari ni moja ya sekta za huduma za jamii hapa nchini, hivyo ni vyema kutimiza majukumu yao ili kuona amani na utulivu uliyopo nchini unaendelea kudumu.
“Vyombo vya habari ni taasisi muhimu katika kukuza na kueneza amani kutokana na kuwa ndio mdomo wa jamii na taasisi zenye mamlaka,”anasema.
Anasema kwa kuzingatia hilo, waandishi walielekezwa kutoshabikia upande wowote miongo ni mwa vyama 17 vilivyojitokeza kushiriki uchaguzi huo lakini pia kuepuka hotuba chonganishi.
“Tuliwataka wanapofanya kazi zao lazima waweke usawa wa nchi na kujizuia kuwa sababu ya kuifanya nchi kuingia katika mtafaruku kwani kufanya hivyo kutasababisha nchi kutokuwepo katika ustawi mzuri,” alisema Mfaume.
Hata hivyo alisema vyombo vya habari vinaaminika sana hivyo kutekeleza majukumu yao ipasavyo itasaidia kuongeza hadhi pamoja na kuzidi kuaminiwa na jamii pamoja na serikali kutokana na umuhimu wao.
Aidha anasema katika kazi zao wanapaswa kuandika taarifa zinazopaswa kubadilisha mitazamo ya wananchi kutoka katika mfumo mzima wa kisiasa na sasa kuelekeza mitazamo yao katika kulijenga taifa kutokana na mambo hayo sasa yameshakwisha.
“Vyombo vya habari ni muhimu na hatari kwani ndivyo vitakavoweza kuifanya amani iendelee au iondoke, hivyo kutokana na maridhiano yaliyopo ni muhimu kuwa chanzo muhimu cha kuendeleza amani hiyo ndani ya nchi,” anasema.
Baadhi ya waandishi waliozungumza na gazeti hili wanasema hivi sasa nchi ipo shwari na wananchi wapo katika kuendesha maisha yao kwa kujitafutia riziki hivyo ni vyema waandishi wasiwe chanzo cha kurudisha majeraha ambayo yashapita.
Wanasema ni vyema waandishi kuandika habari kwa kuzingatia ukweli ili wananchi wabadilike na kudumisha amani.
Wanafahamisha kwamba ikiwa waandishi wataandika kwa kusababisha kuvuruga maelewano yaliyopo itakuwa chanzo cha kuleta migogoro hapa nchini.
“Lazima kazi zao wanazozitoa wazifanyie upembuzi kwa kujua kwamba taarifa hiyo haitokuwa chanzo cha kuondosha amani iliyopo hapa nchini,” anasema Hinja Haji mwandishi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) redio.
Wanasema nchi nyingi zimeingia katika matatizo chanzo kikuu ikiwa ni waandishi hivyo na hapa hatutegemei kufikia huko ni muhimu kuwa makini katika kazi zenu,” anasema.
Yaliyofanywa na serikali katika kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa ni kuendeleza maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa na kuongeza matumaini kwa wananchi.
Hivyo ni vyema waandishi na asasi za kiraia wakaendelea kufanya kazi zao kwa kuendeleza dhamira za maridhiano ya kisiasa ili kuifanya Zanzibar ibaki salaama.
PICHANI JUU: RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi (kushoto), akimkabidhi hati ya kiapo aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Marehemu maalim Seif Sharif Hamad, baada ya kumuapisha hafla iliofanyika katika Ikulu Zanzibar Disemba 12, 2020. (PICHA NA MAKTABA).
Chanzo: Zanzibar leo April 19, 2020.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango