Udhibiti wa migogoro utaimarisha amani, utulivu
NA ASYA HASSAN
IMEELEZWA
kuwa utashi wa kisiasa na mafunzo ya mara kwa mara juu ya udhibiti wa
migogoro utasaidia kuimarisha amani na utulivu nchini.
Meneja wa
shirika la Search for Common Ground, Hussein Faraji Sengu, alieleza hayo hivi
karibuni katika mahojiano na mwandishi wa habari hizi, ofisiani kwake kijangwani,
Zanzibar.
Sengu
alieleza kuwa iwapo makundi mbali mbali ya jamii yatajengewa uwezo, kuna
uwezekano wa hali ya amani kuimarika na kuepuka mizozo.
Alieleza
kuwa ipo mizozo inayoweza kuepukwa kwa wahusika kutambua haki na mipaka yao,
hivyo kupitia mradi wa ‘Dumisha amani Zanzibar’, watakutana na makundi mbali
mbali wakiwemo wanasiasa ili kuwajengea uwezo wa kutambua vichocheo vinavyoweza
kuvuruga amani na utulivu.
“Tunaamini
hatua hii itawafanya wanasiasa kujitambua na kuwasimamia vyema wanachama wao
ili kuepuka migogoro inayotokezea baina yao kabla ya kuwa chanzo cha vurugu,”
alieleza Sengu.
Alisema mfumo
wa vyama vingi uliopo nchini, unaweza kuwa chanzo cha migogoro tofauti, hivyo
kupitia utekelezaji wa mradi huo utaondosha tofauti zilizopo baina ya watu wenye
itikadi tofauti hususani kipindi cha uchaguzi.
“Zanzibar
ni nchi ya amani lakini kuna viashiria hutokezea hususani kipindi cha uchaguzi,
hivyo kukutana na wanasiasa kutasaidia kupata mwamko na umahiri wa kujiepusha
na migogoro inayojitokezea kipindi hicho kwa namna moja au nyengine,” alisema.
Aidha Sengu
alisema wadau wa amani wana nafasi kubwa ya kudumisha amani na kuongeza kasi ya
maendeleo ya nchi na jamii kwa ujumla.
Hata
hivyo alifahamisha kwamba lengo la taasisi hiyo ni kuona wananchi wote wanakuwa
wamoja na wanashirikiana katika kulipeleka mbele kudumu la maendeleo ya nchi
yao.
Akizungumzia
azma ya taasisi hiyo, iliyochangia kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa mwaka
2020, Katibu Mkuu wa chama cha Demokrasia Makini, Ameir Hassan Ameir, alisema
kama wanasiasa watashirikishwa katika mipango ya nchi, watasaidia kuwaelewesha
wafuasi wao juu ya namna bora ya kulinda na kushiriki katika maendeleo ya nchi
yao.
Alieleza
kuwa migogoro mingi inayojitokeza huchangiwa na mgawanyo mbaya wa rasilimali
lakini pia matumizi mabaya ya madaraka hivyo kuna umuhimu wa jamii kujengewa
uwezo kutambua misingi ya mgawanyo wa rasilimali.
“Kinapofika
kipindi cha uchaguzi, kila chama lengo lake ni kupata uungwaji mkono ili
kishike madaraka hivyo kuna haja kubwa ya sisi wanasiasa kujenga uelewa wa
wanachama wetu, kuepuka mizozo ya kisiasa,” alieleza Ameir.
Kwa upande
wake Msaidizi wa Sheria kutoka Jumuiya ya Wasaidizi wa Sheria Zanzibar (ZAPAO),
Fatma Khamis Ali, alieleza kuwa mbali ya wanasiasa, mradi huo unapaswa kuwashirikisha
Wasaidizi wa Sheria kwani wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kutatua migogoro
katika jamii.
“Katika
kazi zetu, tunakutana na aina mbali mbali za mizozo ambayo mengine chanzo chake
ni ukosefu wa uelewa juu ya mambo ya utawala na uongozi sio kwa wanachama au
wananchi tu hata kwa viongozi,” alisema Fatma.
Hivyo
alisema ipo haja ya kutolewa kwa elimu ya uraia kwa wananchi wazijue haki zao ili
wapate kutekeleza wajibu wao kulingana kwa lengo la kuimarisha amani na uwepo
wa serikali ya umoja wa kitaifa.
Mradi wa
‘Dumisha amani Zanzibar’, unatarajiwa kutatua migogoro kwa kuwashirikisha wadau
wakiwemo wanasiasa, asasi za kijamii na viongozi wa dini kuzuia vichocheo vya
migogoro sambamba na kuwa na jamii yenye mwamko wa kuzuia na kutatua migogoro
kabla ya kuleta madhara ili kudumisha amani .
Comments
Post a Comment