Ushirikiano wa vioingozi, wananchi kuimarisha maridhiano
NA MWANDISHI WETU
WANANCHI wa mkoa wa Kaskazini Unguja, wameeleza
kuwa ushirikiano uliopo kati ya viongozi wakuu wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar
umeimarisha maelewano baina ya wananchi hivyo ipo haja ya kuendelezwa.
Wakizungumza na mwandishi nwa habari hizi hivi
karibuni, walieleza kuwa hali hiyo inatokana na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa
Kitaifa (SUK) inayohusisha vyama vya CCM na ACT Wazalendo baada ya uchaguzi
mkuu wa oktoba 28 mwaka uliopita.
Mkaazi wa shehia ya Bumbwini Mafufuni, Haji Nyange
Makame, alieleza kuwa hali hiyo imeongeza kuaminiana miongoni mwa viongozi na
wananchi katika shehia yao.
“Kabla ya uchaguzi, ilikuwa vigumu kumuona
viongozi wa CCM na vyama vyengine wakakaa pamoja katika kazi za kisiasa au
kijamii lakini siku hizi huwezi kumjua nani CCM nani ACT kama mgeni nao,”
alieleza Nyange.
Nae Mwanaacha Hamid Said wa Kilimani Tazari, alieleza
kuwa hali ya ushirikianbo imeongezeka na kupongeza utamaduni ulioanzishwa na
viongozi wa serikali kukutana na wananchi kila siku za Ijumaa.
“Tunawaona Makamu wa wa Kwanza, Makamu wa Pili na
Rais Mwinyi (Dk. Hussein Ali Mwnyi) kila Ijumaa wanakutana na wananchi na kutoa
ujumbe wa maridhiano, umoja na amani. Hili ni jambo linalowanyima nguvu watu
wasiopenda umoja wa Wazanzibari waishi kwa amani,” alieleza mama huyo.
Wananchi hao na wengine, waliwaomba viongozi wa
ngazi za chini kufuata mwenendo wa viongozi hao ili kupata nafasi ya kukutana
na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yao.
Hivi karibuni akiwa katika ziara mkoani humo, Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, alipotembelea wagonjwa na kuzungumza
na wananchi wakiwemo wanachama wa chama cha ACT Wazalendo alisisitiza haja ya
wazanzibari kuendeleza hali ya amani na utulivu iliyopo.
Ziara hiyo iliyoandaliwa na chama hicho, ni sehemu
ya utamaduni uliokuwa ukitekelezwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho,
marehemu Maalim Seif Sharif Hamad.
Akizungumza na wananchi hao kwa wakati maeneo
tofauti, Othman alieleza kuwa Zanzibar inahitaji kuendelea na umoja ili kuharakisha
maendeleo kwa wananchi wake
Alisema hakuna njia nyengine itakayoleta maendeleo
bila kuwepo mashirikiano, upendo na umoja miongoni mwa Wazanzibari.
“Nimeweka ahadi ya kuwatumikia Wazanzibar
wakati wowote ili kuendeleza yale yaliyoanzishwa na kuleta tija katika
muendelezo wa kuyaimarisha zaidi maridhiano ya kisiasa ya Zanzibar,” alisema
Othaman.
Alisema anayo imani kwamba anaweza
kuwatumikia watu wote nchini bila ubaguzi na kufanya kazi kwa moyo ili kuona malengo
ya umoja wa kitaifa yanafikiwa.
“Umoja na upendo ndio silaha pekee itakayodumisha amani
katika taifa letu, inapendeza zaidi kuona watu wakitembeleana na kusaidina kwa
wale wanaohitaji msaada,” alieleza Makamu wa Rais.
Sambamba na hilo aliwashauri wananchi wa Zanzibar kurudisha
utamaduni wa kufutari pamoja kama ilivyokuwa zamzni katika hasa mwezi mtukufu
wa Ramadhani, kwani kufanya hivyo kunaongeza mapenzi baina ya aliyenacho na
asienacho.
“Kuna watu wengi wanaofunga lakini huwa hawana futari,
kama tukiurudisha utamaduni kuftari pamoja ndugu na majirani utaendelea basi utaleta
faida kubwa miongoni mwa jamii,” alieleza Othman.
Katika ziara yake, Othman alifika kuwafariji wagonjwa katika vijiji vya Chaani, Matemwe , Nungwi, Kendwa, Kilimani Tazari, Mahonda, Bumbwini Mafufuni na Kiomba Mvua vya mkoa wa Kaskazini Unguja.
Pichani: MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman (kulia), akizungumza na mzee Mussa Hassan Hassan ambae ni mgonjwa wa muda mrefu alipofika nyumbani kwa mzee huyo kumjulia hali. (PICHA NA OMKR).
Comments
Post a Comment