Wazazi wasiozingatia elimu za
watoto wao kukiona
NA MWANDISHI WETU
MKUU wa Mkoa wa Kusini Unguja,
Rashid Hadidi Rashid, (pichani) amewaagiza masheha wa mkoa huo, kuzidisha mashirikiano na
kutoa taarifa za wazazi wasioshughulikia maendeleo ya elimu ya watoto wao.
Alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia
kuimarisha kiwango cha ufaulu mkoani humo ambacho kwa muda mrefu kipo chini.
Hadidi alitoa agizo hilo skuli ya
Ukongoroni wakati akizungumza na wazazi, walezi, walimu na wanafunzi wa skuli
hiyo.
Alisema imebainika kuwa baadhi ya
wazazi wanapuuza upatikanaji wa elimu kwa watoto wao kwa kushirikisha na
masuala ya ukataji kuni, kujiingiza katika ajira za watoto ikiwemo za kupara
samaki na kupelekea watoto hao kushindwa kuhudhuria skuli kwa wakati, kuwa
watoro na kutodurusu masomo yao.
Alifahamisha kuwa kutokana na hali
hiyo inayofanywa na baadhi ya wazazi kunachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha
nyuma juhudi za serikali juu ya mikakati iliyojiwekea.
Hivyo aliwataka masheha hao
kuwafichua wazazi hao wanaopuuza juhudi hizo ili kuweza kuleta matokeo mazuri
kwa watoto hao sambamba na kuwa na viongozi waliokuwa imara baadae.
Aidha aliwasisitiza wazazi hao kuthamini
juhudi zinazochukuliwa na serikali katika kuimarisha sekta ya elimu na kuwasisitiza walimu wa mkoa huo kuongeza
bidii ya ufundishaji.
“Acheni tabia ya kuzitumia
changamoto zinazowakabili kama ni kigezo cha kushindwa kufaulisha na kupata
matokeo mazuri ya wanafunzi wa mkoa wetu,” alisema Hadid.
Nao wazazi na walimu wa skuli ya
Ukongoroni, walisema miongoni mwa sababu
zinazochangia kwa kutofanya vizuri mitihani yao ya taifa hasa kwa
wanafunzi wa kidato cha nne ni kuwepo kwa mazingara ya imani za kishirikina.
Walisema kutokuwepo kwa mfumo na
sera ya elimu inayoeleweka pamoja na matumizi mabaya ya simu za mikononi na utandawazi
unachangia kukosekana kwa matokeo chanya.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu
Tawala Mkoa wa Kusini Unguja, Salum Kassim Ali, alisema serikali ya mkoa huo imejipanga
kuwapa zawadia walimu watakaofaulisha wanafunzi kwa kiwango cha juu katika
mitihani kwa daraja la kwanza katika masomo yao.
Alieleza kuwa wanafunzi watakaopata
alama ‘A’ hasa kwenye masomo ya sayansi, watapatiwa zawadi ya fedha taslimu shilingi
laki tano kila mmoja kama motisha ya kuwafanya waongeze bidii katika masomo yao.
Comments
Post a Comment