MAADHIMISHO YA MIAKA 57 YA MUUNGANO

Watanzania watakiwa kuulinda, kuutunza, kuuenzi 

  • Makamu wa Rais asema ni tunu na urithi wa taifa

NA MWANDISHI WETU, DODOMA

IMEELEZWA kuwa Watanzania wana kila sabau ya kuulinda, kuuenzi na kuutunza muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar kwa kuwa ni tunu na urithi wa taifa.

Muuungano huo uliotimiza miaka 57 toka ulipoasisiwa Aprili 26, 1964, unatajwa kuwa ni miongoni mwa mambo yaliyoimarisha amani, utulivu na mshikamano miongoni mwa watanzania wa Tanzania bara na Visiwani.

Akilifungua kongamano la maadhimisho hayo katika ukumbi wa Chimwaga jijini Dodoma, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Isdor Mpango alieleza kuwa katika kuimarisha Muungano huo, Serikali  ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zitahakikisha inamaza changamoto 10 zilizobakia baada ya kufanikiwa kutatua changamoto 15 zilizokuwa zinaukabili muungano huo.

Dk. Mpango alisema kuwa serikali mbili hizo zimekuwa zikishirikiana kwa karibu na kuhakikisha wanamaliza changamoto zilizopo kwa manufaa ya wananchi wa pande zote.

"Serikali ya awamu wa sita inayoongizwa na Rais Samia Suluhu Hassan na serikali ya awamu 8 ya Mapinduzi Zanzibar chini ya dk. Hussein Ali Mwinyi, zimedhamiria kumaliza changamoto zilizopo kwa pande zote mbili kwa kuweka kipaumbele suala la muungano katika uongozi wao," alisema Dk.Mpango.

Makamu wa Rais alisema kuwa imekuwa ni tamaduni wetu kuadhimisha sherehe za muungano kitaifa kwa gwaride maalum na burudani katika uwanja mahususi lakini kwa mwaka huu imekuwa tofauti.

"Kutokana na tukio la hivi karibuni ambapo nchi yetu iliondokewa na mmoja wa mashujaa wake Hayati Dk. John Magufuli, aliyekuwa kiongozi mkuu wa taifa letu, tuliamua badala ya sherehe tuadhimishe muungano wetu adhimu kwa kuwa na kongamano hili," alieleza Makamu wa Rais.

Aidha Dk. Mpango alisema kuwa fedha zilizokuwa zitumike katika maadhimisho ya muungano zitapelekwa kwa serikali zote mbili kwa lengo la kuelekezwa katika maendeleo.

"Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watapatiwa fedha hizo kwa ajili ya kuzielekeza katika shughuli za maendeleo," alieleza Makamu wa Rais.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Muungano na Mazingira, Selemani Saidi Jafo, alisema kuwa ili kuifanya jamii iwe na uelewa wa muungano kuna umuhimu wa kutolewa elimu ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa uandishi wa mashindano ya insha kwa wananfunzi wa skuli za msingi na sekondari Tanzania bara na visiwani.

"Jamii bado inatakiwa kuwa na uelewa wa kutosha ju ya muungano kwani bado kuwa mwamko mdogo. Ili kuwepo na uelewa ni muhimu kuwepo na mashindano ya insha ili kuleta hamasa," alisema Jafo.

Nae Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid Salum Mohammed, akilifunga kongamano hilo, alieleza kuwa muungano wa Tanzania ni kielelzo cha umoja na mshikamano wa wananchi wa pande zote mbili za muungano.

Aidha aliwahakikishia watanzania kuwa, serikali zote mbili zitaendelea kuwaletea maendeleo wananchi wake bila ya ubaguzi ili kuenzi misingi ya muungano huo ulioasisiwa Aprili 26, 1964.

“Uwepo wake (muungano) unawanufaisha wananchi wa pande zote mbili ushahidi wa hilo ni uamuzi uliofikiwa wa kupelekwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya sherehe katika shughuli za maendeleo ya jamii,” alisema Dk. Khalid.

Katika kongamano hilo lilohudhuriwa na makundi mbali mbali ya jamii, mada mbali mbali zenye mnasaba na muungano, ziliwasilishwa na kujadiliwa kama moja ya njia za kutambua mchango wa viongozi walioasisi muungano huo, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.  

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango