ZBS
yataja chanzo kupanda gharama ukaguzi bidhaa
NA MWANDISHI WETU
TAASISI ya Viwango Zanzibar (ZBS) imeeleza kuwa gharama kubwa za kuthibitisha ubora wa bidhaa za wajasiriamali inatokana na kutokamilika kwa maabara ya upimaji wa bidhaa za vyakula ya taasisisi hiyo na mlolongo wa vipimo vinavyohitajika kufanyika.
Akizungumza na Waandishi wa habari huko Ofisini kwake Amani, Mkuu wa taasisi hiyo, Rahima Ali Bakari, ameitaja hatua hiyo hupelekea wajasiriamali wengi kushindwa kumudu gharama hizo na kupelekea malalamiko
ya wajasiriamali kutokana na kutomudu gharama hizo.
Alisema
kutokana na hilo, ZBS imeona haja ya kutafuta namna ya kuwasaidia wajasiriamali
hao ili waedelee na kuzalisha bidhaa ikiwa ni pamoja na kuwapa ushauri juu ya
namna ya kuvifikia vigezo na masharti ili kupata alama ya ubora wa bidhaa zao.
“Taasisi
imeamua kuondoa gharama za ukaguzi na kuwashajihisha wawe na maeneo bora ya
kufanyia shughuli zao lakini pia kuwaunganisha na mamlaka nyengine zinazoweza
kuwasaidia kuvifikia viwango vya ubora,” alieleza Rahima.
Akizungumzia
masuala ya vifungashio vya bidhaa za wajasiriamali, Rahima, alifahamisha kuwa
watashauriana na taasisi husika ikiwemo Mamlaka wa viwanda vidogo na vya kati (SMIDA)
ili kuwaendeleza.
Aidha
alisema licha ya kuondolewa kwa gharama za ukaguzi lakini changamoto iliyopo ni
gharama za upimaji wa viwango vya bidhaa za vyakula kutokana na kutokamilika
kwa maabara ya upimaji wa bidhaa za vyakula ya taasisi hiyo.
“Gharama
za upimaji hasa wa bidhaa za vyakula ni kubwa na ZBS inashindwa kuwasaidia
wajasiliamali wote lakini pia wao wenyewe pia hawaziwezi ndio maana tumewaweka
kwenye mpango kazi wetu wa mwaka ujao wa fedha,” alisema Mkurugenzi huyo.
Alieleza
kuwa ili kufikia azma hiyo, ZBS imejipanga kuwatambua wajasiriamali hao na
kuwaweka katika makundi maalum ili iwe rahisi kuwahiudumia ikiwa ni pamoja na
kubeba gharama za upimaji kwa wale watakaokidhi
vigezo.
“Kweli gharama kubwa na wajasiriamali
hawaziwezi, kwa mfano kwenye bidhaa za vyakula, kipimo kimoja kinafika dola za
marekani 50 na bidhaa inatakiwa ifanyiwe zaidi ya vipimo vitatu,” alieleza
Rahima.
Hata
hivyo aliwaomba wajasiriamali kuitumia taasisi hiyo kwa kupata ushauri wa
kitaalamu ju ya uzalishaji wa bidhaa kwa lengo la kukabiliana na changamoto zilizopo
ikiwemo ya kutokuwa na maeneo maalum ya kufanyia biashara zao hali inayopelekea
hata ZBS kupata wakati mgumu wakati wa kufanya ukaguzi bidhaa zao.
Comments
Post a Comment