DC Kati awataka walimu kumaliza mitaala kuongeza ufaulu
NA MWANDISHI WETU
MKUU wa Wilaya ya Kati Unguja, Marina Joel Thomas, amewataka walimu
wa skuli za sekondari Wilayani humo kuhakikisha wanamaliza mitaala kwa wakati
ili wanafunzi wapate muda wa ziada wa kupitia masomo yao.
Marina
alisema hayo katika hafla ya utoaji wa zawadi kwa walimu walioleta ufaulu mzuri
kwa wanafunzi wa kidato cha pili mwaka 2020 iliyofanyika katika ukumbi wa Kituo
cha walimu (TC), Dunga, wilaya ya Kati, mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema
hatua hiyo itasaidia kuongeza fursa kwa wanafunzi kufanya vizuri katika
mitihani yao ya taifa.
“Kumaliza
silabasi mapema kutawasaidia wanafunzi kupata muda mzuri wa kuyapitia masomo yao
na kuongeza ufaulu katika mitihani yao ya taifa,” alisema Marina.
Mbali
na hayo Marina alifahamisha kwamba serikali ya wilaya hiyo imekuwa ikifanya
jitihada kuona kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi kinaongezeka ili kupata
wataalamu wa ndani waliobobea katika fani mbali mbali.
Aidha aliwasisitiza
walimu hao kuendelea kuwa na nidhamu ya kazi sambamba na kuwajibika ipasavyo na
kuwasimamia wanafunzi ili wahudhurie
vipindi kikamilifu.
Akizungumzia
suala la utoro kwa wanafunzi Mkuu huyo wa wilaya, aliwataka walimu na wazazi
kushirikiana kufuatilia myenendo ya watoto wao ili kuleta ufanisi katika eneo
hilo.
Kwa
upande wake Afisa elimu Mkoa Kusini Unguja, Mohamed Haji Ramadhan, aliwashauri
masheha na kamati za skuli kufatilia mwenendo na mahudhurio ya walimu ili kulimarisha
maendeleo ya skuli zao.
Nao
walimu waliopatiwa zawadi hizo waliwashauri walimu wenzao kutenga muda wa ziada
kuwasaidia wanafunzi ili waweza kupata matokeo mazuri na kuleta mabadiliko katika
maendeleo ya elimu skulini mwao.
Comments
Post a Comment