Dk. Mwinyi asema Tanzania inataka dunia yenye amani
NA RAJAB MKASABA, IKULU
JAMHURI ya Muungano wa Tanzania, ikiwemo Zanzibar, zinashirikiana na mataifa mbali mbali katika kudumisha amani, kutafuta suluhu ya migogoro, kuimarisha usalama na maendeleo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi alieleza hayo katika hotuba yake wakati alipoungana na viongozi kadhaa duniani kwa njia ya mtandao kujadili njia za kuimarisha umoja na mshikamano ambapo mada kuu ilikuwa ni “Kuimarisha umoja na kudumisha amani katika rasi ya Korea.
Mjadala huo ambao umefanyika kwa njia ya mtandao kutokana na uwepo wa maradhi ya corona, ambapo Dk. Mwinyi aliimpongeza Dk. Hak Jan Han mwanzilishi wa taasisi ya “Universal Peace Federeration” kwa kumpa fursa ya kuungana na viongozi wengine katika mjadala huo.
Katika mjadala huo ambapo miongoni mwa mambo yaliyozungumzwa ni kuwataka viongozi wa dunia siyo tu kuzungumiza matatizo ya kuzuka kwa maradhi ya COVID 19, bali pia, kuwa na fikra mpya za kuondokana na matatizo yaliyopo na badala yake kuwa wamoja katika hali ya usalama na amani duniani.
Dk. Mwinyi alisema kuwa ingawa kijiografia rasi ya Korea iko mbali na Afrika, lakini ikumbukwe kwamba licha ya umbali huo, Afrika inashiriki kikamilifu katika kurejesha amani katika eneo hilo.
Alisema kwa bahati mbaya, licha ya juhudi zilizochukuliwa na Jumuiya za Kimataifa, eneo hilo bado limebaki na mivutano ambayo inatishia usalama katika eneo la Kusini Mashariki ya Bara la Asia.
“Hatuwezi kuendelea kubaki tunautizama tu mgogoro huo, ambapo baadhi ya wakati unajulikana kuwa ni ‘mgogoro uliosahauliwa, kuendelea kwa mgogoro huo ni kuleta athari nyingi kwa amani na usalama wa dunia”, alisema.
Alitoa pongezi kwa Dk. Han Ja Han, kwa kukusanya timu ya wataalamu kutoka pande mbali mbali za dunia ili waje na rai mpya zenye lengo la kurejesha hali ya amani na usalama ili kuwa na Korea iliyoungana.
Akizungumzia hali ya kisiasa ya Zanzibar na historia yake, Dk. Mwinyi alimpongeza marehemu Seif Sharif Hamad, kwa kukubali kuungana naye katika kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya uchaguzi mkuu.
Alieleza alivyofarajika kwa uamuzi huo wa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambapo ni miongoni mwa mafanikio aliyoyapata ndani ya kipindi kifupi cha miaka mitano atakachokuwepo madarakani.
Dk. Mwinyi alisema kuwa lengo lake ni kuona kuwa kuna Zanzibar ambayo watu wake ni wamoja na inapiga hatua za haraka za maendeleo.
Alisisitiza kwamba Zanzibar imedhamiria kutumia vizuri rasilimali zake na fursa iliyopo kijiografia ya kuwepo eneo la kimikakati na muhimu katika kuendeleza sekta mbali mbali za kiuchumi.
Alifahamisha kuwa serikali anayoiongoza imejidhatiti kuimarisha na kukuza fursa za uwekezaji na kutoa upendeleo maalumu kwa wawekezaji wanaowekeza kisiwa cha Pemba ili kukuza maendeleo katika kisiwa hicho.
Aidha, alisema kuwa Zanzibar ina fursa na rasilimali nyingi za kuendeleza uchumi imara utakaoweza kukuza ajira, kupunguza umasikini na hatimae kupata maendeleo ya haraka.
Aliongeza kuwa Zanzibar imedhamiria kuendeleza uchumi wa buluu kwa kushirikiana na nchi wanachama wa jumuiya ya nchi zinazopakana na bahari ya Hindi (IORA) ambazo nazo kwa upande wao zimepanga kuendeleza uchumi huo.
Dk. Mwinyi alieleza kwamba serikali itahakikisha katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo inashirikiana na washirika wa maendeleo ili kufikia malengo yake ya kukuza ajira, kuimarisha sekta ya elimu, afya, na miundombinu kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya Mwaka 2050.
Dk.
Mwinyi alimuunga mkono Dk. Hak Jan Han, pamoja na wanachama na marafiki wote wa
taasisi ya “Universal Peace Federation” na Jumuiya zake katika kuimarisha amani
na kuharakisha maendeleo.
Comments
Post a Comment