Dk. Mwinyi ahimiza waumini kufanya hijja mapema
NA MWANDISHI WETU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi, amewataka waumini wa dini ya kiislamu kujipanga
na kufanya ibada ya Hijja mapema badala ya kusubiri hadi baada ya kustaafu.
Aidha aliieleza kuwa serikali inaendelea
na mikakati ya kuanzisha mfuko wa Hijja ili kuwafanya waumini wengi kutekeleza
ibada hiyo ambayo ni nguzo ya tano ya Uislamu.
Dk. Mwinyi, aliyasema hayo jana alipokuwa
akihutubia katika baraza la Eid el Fitri katika ukumbi wa Sheikh Idrissa
Abdulwakil, Kikwajuni Mjini Unguja, baada ya waumini wa dini ya kiislamu
kumaliza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Alisema Mahujaji wa Zanzibar
wanapaswa kujiandaa mapema kuteleza ibada hiyo, badala ya kusubiri hadi mtu
anapostaafu na ameitaka Kamisheni ya wakfu na Mali ya Amana, kukamilisha
mapendekezo yaliotolewa ili kufanikisha mfuko wa Hijja Zanzibar.
Alisema ili kutekelelza vyema ibada
hiyo na kuuendeleza mbele uislamu serikali imeamua kuanzisha mfuko huo utaowasaidia
waislamu kufanya ibada hiyo kwa wakati mzuri na sio kusubiri wanapostaafu ndipo
waende hijja.
Hata hivyo, alisema katika mwaka
2020, waislamu walishindwa kufanikisha ibada ya Hijja ya kwenda Makka nchini
Saudi Arabia kutokana na zuio la ugonjwa wa Covid -19.
“Serikali inafuatilia kwa karibu jambo
hili na inakusudia kuweka mazingatio maalum kwa mahujaji walioweka nia ya
kutekeleza ibada hiyo mwaka huu, ili kuwawezesha kufanikisha jambo hilo na
kukidhi masharti yatakayowekwa,” alieleza Dk. Mwinyi.
Sambamba na hayo alieleza kuwa hivi
karibuni serikali itatoa taarifa za ziada ili kukidhi masharti yatakayowekwa na
kuwaahidi mahujaji wa Zanzibar, kukaa tayari kwani serikali inafanya
mawasiliano na serikali ya Saudi Arabia ili kuona vigezo vinavyovitakiwa kwa
mahujaji vinafuatwa.
Akiendelea Rais Mwinyi, aliwataka viongozi
na vyombo vya sheria nchini, kuingiwa na hofu ya Mungu kwa kuhakikisha
wanatenda mambo mema katika uwajibikaji wao ili kuwasaidia wanyonge kupata haki
zao.
“Uadilifu tukiuendeleza, utaimarisha
utoaji wa haki, utaweka usawa katika kupata huduma na ni msingi muhimu wa
sheria na utawala bora,” alisema.
“Kwa hivyo, ili jamii yetu iondokane na
vitendo mbalimbali vinavyowanyima haki miongoni mwetu na hasa wananchi
wanyonge, viongozi sote, watumishi wa umma na watendaji katika vyombo vya
sheria tuna wajibu wa kutekeleza majukumu yetu kwa uadilifu,” alisema Dk.
Mwinyi.
Alisema katika kipindi cha mwezi
mtukufu wa Ramadhani, wananchi wengi walionekana kubadili tabia kwa kuishi
kufuata misingi ya uadilifu, jambo ambalo linahitaji kuendelezwa ili nchi
iendelee kubaki ikiwa katika umoja, amani na utulivu.
Alisema huruma iliyooneshwa na wananchi wenye nacho
kuwapa watu wanyonge, inahitaji kuendelezwa, kwani bado Zanzibar inakabiliwa na
makundi ya wazee, wajane, yatima wasiojiweza,
walemavu, watoto waliotelekezwa, mafukara, na makundi mengine yanayohitaji
misaada kutoka kwa wenye uwezo ili nao washerehekee sikukuu wakiwa na furaha.
Alisema inafurahisha kuona vijana
wengi ndani ya mwezi huu, wameonyesha uwezo wao wa kusoma quraani katika
mashindano mbali mbali yaliofanyika hapa nchini, jambo ambalo linahitaji
kuendelezwa ili kuwafanya vijana wa Zanzibar kuwa wenye maadili mema.
Mapema akitoa hotuba ya baraza
hilo, Juma Ngwali Juma, alisema suala la umoja ni jambo linalosisitizwa katika
uislamu na vyema waumini wa dini hiyo wakaona umuhimu wa kuendeleza yale yote
waliyojifunza katika mwezi wa Ramadhani.
Akimkaribisha Dk. Mwinyi, Waziri wa
Nchi, ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala bora, Mwalimu
Haroun Ali Suleiman, alieleza kuwa wananchi wa Zanzibar wameonesha utiifu wa
hali ya juu wakati wa mwezi mtukufu wa ramadhani hali iliyopelekea kuimarika
kwa hali ya amani na utulivu nchini.
Aidha alisema wananchi wengi
walivutiwa na utaratibu alioufanya dk. Mwinyi wa kushirikia nnao katika matukio
mbali mbali ya kiibada jambo ambalo linastawisha imani na mshikamano miongoni
mwao.
“hali hii imaeongeza imani ya
wananchi kwako (Dk. Mwinyi), kwani mbsali ya kuwafutarisha wananchi wa mikoa
mitano ya Zanzibar kama ilivyokuwa kwa watangulizi wako, ulishiriki nao katika
sala za tarawehe kwenye ,misikiti mbali mbali jambo lililowafanya waendelee
kukuamini na kukuombea dua,” alieleza mwaliu Haroun.
Baraza hilo lilihudhuriwa pia na
viongozi mbali mbali wa serikali zote mbili za Tanzania waliopo madarakani na
waliostaafu, watendaji wa ngazi mbali mbali na mume wa rais wa jamhuri ya
muungano nwa Tanzania, Maalim Hafidh Ameir.
Comments
Post a Comment