Hemed Mgeni Rasmi maadhimisho uhuru wa habari Z’bar
NA MWANDISHI WETU
MAKAMU wa Pili wa Rais wa
Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika
maadhimisho ya siku ya uhuru wa habari kitaifa yatakayofanyika mwishoni mwa
wiki hii katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, Zanzibar.
Akizungumza katika mkutano wa
waandishi wa habari, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya maadhimisho
hayo, Dk. Mzuri Issa Ali, (wa pili kulia) alieleza kuwa maadhimisho hayo yatafanyika Jumapili Mei 30, 2021 na zaidi ya watu 250 wakiwemo waandishi wa habari, wadau wa habari na
wawakilishi wa taasisi za umma na asasi za kiraia wanatarajiwa kuhudhuria.
Alieleza kuwa maadhimisho hayo yataambatana
na uwasilishaji wa mapendekezo ya mswada ya sheria mpya ya habari Zanzibar ulioandaliwa na
wadau wakiwemo waandishi wa vyombo mbali mbali vya binafsi, serikali na
mashirika ya habari.
“Mswaada huo ambao umebeba miongozo
na maazimio ya habari kikanda, kimataifa na kuzingatia mazingira ya Zanzibar,
umekamilika na unategemewa kukabidhiwa rasmi kwa Mhe. Makamu wa Pili akiwa
ndiye Mtendaji Mkuu wa shughuli za Serikali nchini,” alieleza Dk. Mzuri.
Aliongeza kuwa mswada huo unapendekeza
kufuta sheria namba 5 ya Magazeti ya mwaka 1988 na vifungu vya sheria nyengine
vinavyooana navyo ambavyo vimepitwa na wakati na pia haviweki mazingira mazuri
kwa sekta ya habari na wanahabari kufanya kazi vizuri.
Alisema shughuli nyengine ni utoaji
wa tuzo za uandishi wa umahiri na weledi kwa waandishi wa habari ambao
waliwasilisha kazi zao katika kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo.
Alizitaja tuzo zitakazokabidhiwa
kuwa ni ya tuzo ya uandiahi wa habari za uchumi wa buluu iliyopewa jina la tuzo
ya Dk. Mwinyi, tuzo ya uandishi wa habari za serikali ya umoja wa kitaifa,
inayoitwa tuzo ya Maalim Seif na tuzo ya habari za jinsia ijulikanayo kama tuzo
ya Mama Maryam Mwinyi.
Aidha Dk. Mzuri, alizitaja tuzo
nyengine kuwa ni tuzo ya habari za rushwa na uhujumu uchumi (tuzo ya ZAECA)
ambayo itatolewa pia kwa kwa mshindi wa
pili na wa tatu na tuzo ya habari za Kodi (tuzo ya ZRB) ambapo jumla ya kazi 52
zimewasilishwa.
alieleza kuwa kazi hizo
zitatangazwa na kuoneshwa ili iwe kujenga uelewa na hamasa kwa waandishi wa
habari kufanya kazi nyingi zitakazowasilishwa katika maadhimisho ya mwaka
unaofuata kwa vile tuzo hizi zinatarajiwa kuwa endelevu.
Pia Mzuri alizishukuru taasisi na
wadau mbali mbali waliojitokeza kuunga mkono maandalizi ya maadhimisho hayo na
kuwaomba wadau wengine kujitokeza kushirikiana na taasisi zinazoandaa
maadhimisho hayo.
Alizitaja taasisi zinazoshirikiana
kuandaa maadhimisho hayo kuwa ni pampoja na Baraza la Habari Tanzania (MCT) Ofisi
ya Zanzibar, Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo (WAHAMAZA), Klabu ya
Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), Klabu ya Waandishi wa Habari Pemba (PPC), Idara
ya Mawasiliano na Mafunzo ya habari ya Chuo Kikuu cha taifa Zanzibar (SUZA) na Chama
cha waandshi wa habari Tanzania (TAMWA) ofisi ya Zanzibar
Maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Habari
Kimataifa huadhimishwa Mei 3 ya kila mwaka lakini Zanzibar taaisisi
zinazoratibu na kuandaa maadhimisho hayo ziliakhirisha ili kupisha mwezi
mtukufu wa Ramadhani.
Comments
Post a Comment