Sadaka zinaimarisha amani, upendo kwenye jamii – Sheikh Kahalid
NA MWANDISHI WETU
OFISI ya
Mufti wa Zanzibar imeeleza kuridhishwa kwake na sadaka zinazotolewa kwa watu
wenye mahitaji maalum na watoto yatima, kwani inasaidia kuimarisha amani, upendo
na kupunguza ukali wa maisha miongoni mwa jamii.
Katibu wa
ofisi hiyo Sheikh Khalid Ali Mfaume, alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza
wakati wa zoezi la ugawaji wa vyakula vya futari iliyotolewa na taasisi ya
Shura Muslim Charitable Organization katika ofisi za jumuiya hiyo, Kilimahewa,
mjini Zanzibar.
Alisema
Mweyezi Mungu aliyataja makundi ya mayatima, wajane na watu wasiojiweza kuwa
miongoni mwa yanaopaswa kusaidiwa hivyo jumuiya hiyo imefanya jambo jema
linalopaswa kuigwa na kila mwenye uwezo.
“Tumehimizwa
na Allah (S.W) kuwashika mkono mayatima, masikini na wale wenye mahitaji maalum
kwani kufanya hivyo sio kunawapunguzia ugumu wa maisha tu, bali huongeza upendo
na kujenga amani katika jamii,” alisema Sheikh Mfaume.
Alisema
jamii isiyokuwa na usawa, watu wake wanakosa utulivu wa nafsi na kuwa sababu ya
kuoneana choyo na husda hivyo ipo haja kwa kila mmoja kujenga utamaduni wa
kutoa sadaka kwa kadri ya uwezo alionao.
Aidha
aliwashukuru wafadhili ya jumuiya hiyo, Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE)
kwa kufadhili futari na shughuli za jumuiya hiyo ambayo imekuwa ikitoa misaada
mbali mbali ikiwemo ya elimu kwa watoto mayatima.
Awali
akizungumza katika zoezi hilo, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Juma Ali Khamis,
alieleza kuwa jumla ya msaada huo ni mwendelezo wa misaada inayotolewa na
jumuiya yake kwa familia zinazolea watoto yatima, wazee na watu wanaoishi
kwenye mazingira magumu.
Aliongeza
kuwa kabla ya kutoa msaada wa futari kwa wananchi wa Unguja, walifanya hivyo
katika maeneo mbali mbali ya kisiwa cha Pemba pamoja na kufutarisha katika
maeneo ya Unguja ambapo zaidi ya watu 4,000 wamenufaika.
“Toka
jumuiya yetu ilipoanzishwa mwaka 2014 tumekuwa na harakati zinazoyahusu makundi
haya na kwa mwaka huu Alhamdulillah tulianza kwa kutoa sadaka ya vyakula vikavu
kule Pemba na sasa tupo hapa Unguja,” alieleza maalim Juma.
Aliyataja
maeneo yaliyofikiwa na idadi ya watu waliofikiwa kwenye mabano ni Msuka (200),
Wingwi (300, Pandani (165), Shengejuu (700), Mvimbe Pandani (65) kwa upande wa
kisiwa cha Pemba ambapo katika kisiwa cha Unguja familia 150 zimefikiwa.
Nae mmoja
ya wanufaika wa sadaka hiyo anaetunza watoto saba mayatima wakiwemo wanawake
wanne, aliwashukuru wafadhili waliofanikisha kupatikana kwa sadaka hiyo na
viongozi wa jumuiya ya Shura kwa kuwapatia msaada huo ambao alisema utawasaidia
kupunguza ugumu wa maisha.
“Tunashukuru
vyakula hivi vitatusaidia kupata utulivu katika maswala ya chakula katika
kipindi hiki cha ramadhani na kile kipato kdogo tulichonacho tutakitumia kwenye
maswala ya mavazi ingawa bado tunaomba tusaidiwe na huko,” alieleza mama huyo
ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini.
Katika hafla hiyo zaidi ya familia 150 zinazoishi na watoto yatima, wazee wasiojiweza na wanaoishi kwenye mazingira magumu walipatiwa futari hiyo iliyojumuisha mchele, maharage, mafuta ya kula, sukari, unga wa ngano na tende.
Comments
Post a Comment