Wanahabari watakiwa kuibua changamoto za jamii

NA ASYA HASSAN

WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kusimamia wajibu wao wa kuibua changamoto zinazowakabili wananchi ili ziweze kupatiwa ufumbuzi wa haraka.

Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa kaskazini Unguja, Makame Haji Machano, alipokuwa akifumngua mkutano wa wadau kuadhimisho ya siku ya uhuru wa habari duniani kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Ayoub Mohammed Mahmoud.

Mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za mkoa huo Mkokotoni, wilaya ya Kaskazini 'A', Unguja uliandaliwa na klabu ya waandishi wa habari Zanzibar (ZPC) na kuhudhuriwa na wanachama wa klabu hiyo, viongozi wa asasi za kiraia, taasisi za umma na biashara.

Makame alieleza kuwa waandishi wa habari na vyombo vya habari ndio mdomo wa jamii hivyo wakitekeleza vyema majukumu yao, watawasaidia viongozi kujua mahitaji ya wananchi na kuwatimizia kwa wakati.

Alifahamisha kwamba watu wote ikiwa viongozi au raia wa kawaida wanahaki ya kupata habari kutokana na eneo hilo ni muhimu katika kuleta mustakabali mwema wa taifa.

Aidha katibu tawala huyo, aliviomba vyombo vya habari kutanua wigo na kuweka wawakilishi wao ndani ya mkoa huo ili kurahisisha upatikanaji wa habari na taarifa na kupelekea utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi.

“Sote tuanakiri kwamba waandishi wa habari mnawajibu mkubwa wa kuchangia maendeleo ndani ya jamii, hivyo uwepo wenu na hata ulinzi wa uhuru wenu ni jambo la lazima hivyo nawahakikishia kwamba ofisi nyetu itahakiksha inafanya kazi karibu nanyi lakini pia kuondoa vikwazo katika kazi zenu,” alisema Makame.

Alisema waandishi wa habari ni mdomo wa jamii na wanaifikia kwa asilimia kubwa hivyo ni vyema kufanya hivyo ili kuona malengo ya Mkoa huo yanafanikiwa na kuleta tija hapa nchini.

Sambamba na hayo alisema Ofisi hiyo imejiwekea mikakati mbalimbali katika kuwatumikia wananchi katika mambo muhimu ya kijamii.

"Ofisi imejipanga ndani ya kipindi cha uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kuondosha hali duni za wananchi pamoja na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii ikiwemo maji, afya, elimu na nyenginezo ziwezekupatikana kwa urahisi," alisema.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari Zanzibar (ZPC), Abdallah Abdulrahman Mfaume, alisema lengo la kuadhimishwa siku hiyo ni kutathmini mafanikio na changamoto zinazowakabili waandishi pamoja na kusisitiza haja ya serikali kurahisisha upatikanaji wa taarifa ili kurahisishia utendaji kazi za kila siku.

Alisema mchango wa waandishi wa habari katika maendeleo na ustawi wa jamii ni mkubwa hivyo ipo haja ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na kuleta maendeleo kwa taifa.

“Kuna umuhimu mkubwa kwa taasisi mbali mbali za serikali na binafsi kuwa na waandishi wa habari ili kutangaza kazi ya taasisi hizo hatua ambayo itarahisisha upatikanaji wa taarifa na kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayoikabili jamii,” alieleza.

Akisoma salamu za Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Naibu Katibu Mkuu wa ZPC, Mwajuma Juma Kombo, alisema Sweden inatambua na kuthamini kazi ya waandishi wa habari kwa kuwa ni haki ya msingi katika jamii inayoheshimu demoklasia.

Alisema maendeleo ya nchi yoyote yanapatikana kwa kupeana taarifa pamoja na kujadili kwa uwazi na kuwajibishana mambo yanayowahusu.

"Sisi tutaendelea kuungana na Watanzania wote katika jitihada za kukuza na kuendeleza uhuru wa habari hapa nchini, " alisema.

Kwa upande wa washiriki mkutano huo kutoka asasi za kiraia walisema vyombo vya habari vina mchango mkubwa wa kuleta maendeleo kutokana na kuwa mstari wa mbele kuzitangaza asasi hizo katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Umuhimu wa vyombo vya habari haupo kwenye wartu kupata habari pekee, bali vyombo vya habari vinachangia katika ulinzi wan chi na ustawi wa jamii, hivyo ipo haja ya kundi hili kulindwa na kuthaminiwa,” alisema Makurugenzi wa kampuni ya Rom Solutions, Viorica En Escu.

Maadhimisho ya siku ya uhuru wa habari duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo Mei 3 kila mwaka ambapo ZPC iliunganga na klabu nyengine nchini Tanzania kuiadhimisha siku hiyi juzi, wakati kitaifa Zanzibar maadhimisho hayo yatafanyika Mei 22 na 23, mwaka huu.

1.MWENYEKITI wa Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), Abdallah Abdulrahman Mfaume, akihutubia katika mkutano wa wadau wa habari kuadhimisha siku ya uhuru wa habari duniani uliofanyika katika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Kaskazini Unguja, Mkokotoni. (PICHA NA HAROUB HUSSEIN).

MKURUGENZI wa kampuni ya Rom Solutions Ltd, Viorica En Escu, akiwasilisha salamu za taasisi yake katika mkutano wa kuadhimisha siku ya uhuru wa habari duniani uliofanyika katika ofisi za Mkuu wa mkoa wa Kaskazini Unguja. (PICHA NA HAROUB HUSSEIN).
Baadhi ya waandishi wa habari, wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar na wadau wa klabu hiyo wakifuatilia hotuba ya Katibu Tawala wa mkoa wa Kaskazini Unguja, Makame Haji Machano (hayupo pichani), alipokuwa akifungua mkutano wa kuadhimisha siku ya uhuru wa habari duniani,  uliofanyika katika ofisi za Mkuu wa mkoa wa Kaskazini Unguja. (PICHA NA HAROUB HUSSEIN).

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango