Madiwani watakiwa kuchochea matumizi baraza watumiaji nishati
NA MWANAJUMA MMANGA
MADIWANI wa Mkoa wa Kaskazini Unguja wametakiwa kuwahamasisha
wananchi kulitumia Baraza la Watumiaji wa Huduma za maji na nishati (CRC) kueleza matatizo
yanayowakabili katika vijiji vyao kupitia sekta hizo.
Akitoa
mafunzo kwa madiwani hao, Katibu Mtendaji baraza hilo, Hadia Abdulrahman Othman huko Mkokotoni, alisema lengo la serikali
kuunda baraza hilo ni kulinda na kusimamia maslahi ya watumiaji kwa kuhakikisha
matatizo yanayowakabili katika sekta za maji, umeme, mafuta na gesi yanapatiwa
ufumbuzi.
Aliwataka
madiwani hao kuzingatia taratibu zote za kisheria za uungaji na
matumizi sahihi ya huduma za maji na nishati ili ziwe endelevu na salama
kwa wananchi.
“Niwaombe
sana Madiwani kuhakikisha uungaji wa maji na nishati ya umeme unakuwa kwa
mujibu wa sheria na akanuni zilizoekwa na serikali ili kuepusha kupotea kwa mapato
ya seriakli sambamba na kuepusha malalamiko yanayojitokeza,” alieleza Hadia.
Hivyo
aliwasihi wananchi kuacha tabia ya kujiungia kienyeji huduma hizo badala yake
kufuata taratibu zilizowekwa na mamlaka husika ili kuondoa malalamiko yasiokuwa
ya lazima.
Nao
washiriki wa mafunzo hayo waliwaomba viongozi wa baraza hilo kuweka mawakala
katika wilaya zote ili wananchi wapeleka malalamiko yao kwa urahisi kutokana na
umuhimu wa huduma hizo.
“Sisi
wananchi tutajitahidi kufata maelekezo ya kujiunga na huduma hizo na kufuata sheria
zilizowekwa kwani hakutakuwa na vikwazo vyovyote vile na kuwataka wezetu
kupunguza migongano baina ya ZAWA na ZURA,” walisema.
Mafunzo
hayo ni sehemu ya utaratibu wa baraza hilo kujenga uelewa wa wadau wake na
wananchi ili waweze kulitumia kutoa malalamiko kuhusiana na utendaji wa taasisi
zinazojihusisha na utoaji wa huduma za maji, nishati ya umeme, mafuta na gesi
asilia nchini.
Comments
Post a Comment