SMZ yavutiwa na nia ya BOSCH kuwekeza Z'bar

NA MWINYIMVUA NZUKWI

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imeeleza utayari wake kushirikiana na kampuni ya BOSCH Groups ya Ujerumani kuwekeza katika nyanja mbali mbali za uchumi nchini.

Wakizungumza kando ya mkutano wa utambulisho na Rais wa kampuni hiyo kanda ya Afrika, Dk. Markus Thill, Waziri wa Nchi ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaban, walieleza kuwa serikali ipo tayari kuisaidia kampuni hiyo kufikia malengo.

Walieleza kwamba, ili kuimarisha kasi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya uwekezaji nchini, serikali imeona vyema kuweka mazingira yatakayohamasisha uwekezaji.

"Ujio wa BOSCH nchini utavutia wawekezaji wengine kufikiria kuja na kuwekeza nchini wakiamini kwamba watapata huduma stahiki kutokana na uzoefu wake katika uwekezaji ndani na nje ya Afrika," alieleza Soraga.

Aliongeza kuwa mbali ya kutenga maeneo maalum ya uwekezaji na kuweka vivutio vikiwemo vya kikodi, uwepo wa kampuni zinazozalisha vifaa na teknolojia ya kisasa, huchochea kasi na ongezeko la miradi ya uwekezaji na kuongeza fursa za ajira na ukuaji wa uchumi.

Aliongeza kuwa katika kikao hicho, Rais huyo alieleza shughuli mbali mbali zinazofanywa na kampuni hiyo ambazo alisema kuwa zinaweza kuwekezwa nchini hivyo wameikaribisha kwa kutambua maeneo na shughuli zinazoweza kuwekezwa nchini.

Nae Waziri Shaaban, alieleza kuwa Zanzibar inahitaji makampuni makubwa yatakayowekeza katika viwanda vya teknolojia ya habari na mawasiliano na vipuri vya magari na mitambo hatua ambayo itaongeza kasi ya ukuaji uchumi na maendeleo ya nchi.

"Ili kukuza weledi na uwezo wa nyanja mbali mbali ni lazima kuwa tayari kualika uwekezaji wa kampuni kubwa na zenye uzoefu mkubwa ili kuimarisha viwanda ambavyo vitazalisha ajira," alisema Shaaban.

Awali akizungumzia ujio wa kampuni hiyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watoa Huduma wa Sekta ya Mafuta na Gesi (ZAOGS), Balozi Abdulsamad Abdulrahim, alisema kampuni hiyo iliyowekeza katika nchi mbali mbali ulimwenguni imeonesha nia ya kushirikiana na SMZ katika kutekeleza malengo ya maendeleo ya Zanzibar 2050.

“Kampuni hii tayari imewekeza Euro 230,000 kwenye vifaa vya karakana ya magari jijini Dar es salam, kituo hicho kinawezesha upatikanaji wa vifaa na huduma za magari na ujuzi vitu vinavyoweza kuanzishwa hapa Zanzibar na kuajiri vijana wetu,” alieleza Abdulsamad.

Akizungumzia ujio wake, Dk. Thrill, alipongeza ukarimu wa viongozi wa Zanzibar na kueleza kuwa kampuni hiyo mbali ya kuwekeza itatoa mafunzo kwa vijana ili kuweza kuingia katika soko la ajira.

“Tumefanya hivyo katika maeneo mengi barani afrika kulingan nan a mahitaji. Hili ni jambo la maana zaidi kwani uwekezaji katika rasilimali watu ni bora zaidi kuyliko vitu,” alisema Dk. Thrill.

Kundi la makampuni ya BOSCH ni miongoni mwa makampuni yanayotoa huduma za teknolojia ambayo imeajiri zaidi ya watu 375,000 ulimwenguni kote ambayo katika mwaka 2015 ilifanya mauzo ya bidhaa na ujuzi yenye thamani ya Euro bilioni 70.6.

Comments

Popular posts from this blog

ZALIRI, FLI zaingia makubaliano kuimariusha sekta mifugo

Ibueni changamoto zinazokamisha usawa wa kijinsia - Simbaya

Uislam unakubali uzazi wa mpango